dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 27, 2012

Ilikuwaje chama kikampindua Rais Aboud Jumbe ?

Mhe Aboud Jumbe Mwinyi
Na Joseph Mihangwa
Raia Mwema no.226
Tarehe 15 February 2012.

WAKATI alipokubali kuunganisha chama chake cha Afro-Shirazi (ASP) na chama cha Tanganyika African Union, Oktoba 1976, Rais wa Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, hakujua kwamba kwa kufanya hivyo, alikuwa anajitia kitanzi cha kupoteza urais wa Zanzibar miaka minane baadaye.

Tangu mwanzo, chale zilimcheza Jumbe, pale Mwalimu Julius Nyerere, Septemba 5, 1975, alipopendekeza kwenye kikao cha pamoja cha Halmashauri Kuu [NEC] za TANU na ASP, kwamba vyama hivyo viungane.
Lakini Jumbe, kwa kusita, na kwa hofu na shaka iliyofichika, alitaka chama chake kipewe muda zaidi kuweza kufikiria pendekezo hilo.

Hatimaye, makubaliano ya Oktoba 1976 yalizaa chama kipya kilichoitwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichozinduliwa Februari 5, 1977. Ni CCM
kilichompiga buti Jumbe, Januari 1984, kwa tuhuma za kuthubutu kuhoji muundo wa Muungano, akapoteza nafasi zote za uongozi – urais wa Zanzibar, umakamu mwenyekiti wa CCM Taifa, na umakamu wa rais wa Muungano. Ilikuwaje?

Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi aliongoza Zanzibar kuanzia Aprili 1972 baada
ya kifo kwa kupigwa risasi cha Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani
Karume. Alirithi nafasi hiyo kwa msaada mkubwa wa Mwalimu Nyerere
dhidi ya matakwa ya baadhi ya Wazanzibari ambao walitaka mtu mwenye
kuenzi na kuendeleza fikra na utawala wa kibabe wa Karume, arithi
nafasi hiyo. Walimtaka Kanali Seif Bakari.

Mwalimu hakukubaliana na maoni ya Wazanzibari ya kumteua Kanali Seif
Bakari, mwanajeshi, kuwa Rais wa Serikali ya awamu ya pili, Zanzibar.

Alijenga hoja kwamba, kwa kuwa Karume aliuawa na mwanajeshi, Luteni
Hamud Hamud, kumteua mwanajeshi mwingine (Bakari) kuwa Rais, kungeleta
picha na hisia kwamba, kuuawa kwa Karume yalikuwa ni mapinduzi ya
kijeshi.

Nyerere akampendekeza aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Rais (mambo ya
Muungano), Aboud Jumbe, kuchukua nafasi hiyo. Hoja yake ikapita.

Jumbe na Nyerere walifanana kwa mengi: wote walikuwa wasomi waliosoma
pamoja Chuo Kikuu Makerere; kisha wote wakawa waalimu. Jumbe alilegeza
mengi yenye ukakasi yaliyokithiri wakati wa utawala wa Karume. Hata
ile misuguano iliyotia fora kabla ya hapo, kati ya Karume na Nyerere
juu ya Muungano na kutishia kuvunjika kwa Serikali ya Muungano,
ilitoweka.

Hatimaye Jumbe alianza kukubalika Visiwani na Bara; akawa kipenzi cha
Rais wa Muungano, Mwalimu Nyerere. Mara nyingi alialikwa Bara na
baadaye akapaona kama nyumbani kwake.

Lakini kadri alivyozidisha ziara za kirais Bara na nje ya nchi
kumwakilisha Nyerere, ndivyo alivyozidi kujitenga na siasa pamoja na
mambo mengi ya Visiwani. Hatimaye alipaona Dar es Salaam kuwa kwake
zaidi kuliko Zanzibar. Aliweza kuruka kwa ndege kwenda Zanzibar mchana
kwa ziara fupi, na kurejea Dar jioni.
Kutokuwepo kwake Zanzibar kwa muda mrefu kulizua pengo na ombwe la
kiuongozi kwa kuwa hakuna miongoni mwa wasaidizi wake aliyethubutu
kumfuata Dar Es Salaam kwa mashauriano. Kwa sababu hii kila kitu
kilisubiri arudi Zanzibar kwa “ziara” fupi, hata kama ni idhini ya
kukata mti.
Nyerere alifurahishwa na utendaji wa Jumbe na kuingiwa hamu ya kutaka
Muungano zaidi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ikiwa ni pamoja na
uwezekano wa kuviunganisha TANU na ASP, kama tulivyoona mwanzo.
Ili kumfurahisha Mwalimu Nyerere juu ya Muungano, mara nyingi hotuba
zake zilianza hivi: “Tunataka umoja; ni kwa njia hii pekee kwamba
tunaweza kubadili mambo mengi, ili kwamba palipo na kukata tamaa pawe
na matumaini, penye chuki pawe na upendo na amani……”.
Muungano ulivyozidi kuimarika, ulifika wakati Jumbe akajiona kama
mrithi halali mtarajiwa wa Rais Nyerere, na hivyo kujimwaga zaidi roho
na mwili kwa mambo ya Muungano, badala ya kushughulikia utawala wa
Visiwani. Ni matarajio hayo ya kurithi nafasi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano, yaliyomfanya akubali kirahisi kuungana kwa ASP na TANU.
Ingekuwa enzi za Karume, na kwa jinsi tofauti kati yake na Nyerere
zilivyokuwa dhahiri na kubwa, huenda TANU na ASP visingeungana.
Kuanzia Februari 1972 hadi Aprili 1983, Chama kipya – CCM kilifurahia
ndoa mpya kwa utulivu; lakini pale Nyerere alipopendekeza marekebisho
zaidi ya “kuimarisha Muungano”, mlipuko mpya wa malalamiko ulitokea
Zanzibar, moja ya hayo ni hofu ya nchi hiyo kumezwa na “Tanganyika”.
Hofu ya Wazanzibari iliongezeka pale Watanzania Bara walivyozidi
kupendekeza kuwa na Serikali moja ya Muungano, badala ya muundo wa
Serikali mbili ndani ya Muungano. Hofu hizi za Wazanzibari zilianza
kumweka pabaya Jumbe juu ya uswahiba wake na Nyerere; alianza kuitwa
“msaliti” wa Wazanzibari na Zanzibar, naye akaanza kugeuka nyuma,
lakini kwa kukanganyikiwa; alikuwa njia panda.
Ili kurejesha imani ya Wazanzibari kwake, lakini kwa chukizo kwa
Nyerere, Jumbe aliomba mawazo ya kiserikali kutoka kwa makatibu wakuu
wote wa wizara na watendaji wakuu wengine wa Serikali ya Zanzibar.
Wote walikataa muundo wa Muungano wenye Serikali moja, wakapendekeza
kuwe na Serikali tatu – Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar
na Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano tu. Lakini kubwa
lililomchanganya akili Jumbe lilikuwa njiani, likimnyemelea.
Mwaka 1983, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Muungano, Edward
Moringe Sokoine, aliteuliwa kuwa waziri mkuu. Sokoine alikuwa kiongozi
makini, shupavu, mnyoofu na mwenye mvuto mkubwa kwa watu. Na katika
kipindi kifupi tu, alijidhihirisha kuwa “chaguo la watu” na mrithi
halali wa Nyerere ambaye naye alimkubali kwa ishara na kwa vitendo.
Akawa anaonyesha upendeleo dhahiri kwa Sokoine. Kuna sababu nyingi kwa
hilo; lakini itoshe kutaja tatu tu kati ya hizo.
Moja ni kwamba, Nyerere alianza kumwona Jumbe kama kiongozi mpweke,
asiyeungwa mkono na watu wa chini (umma) Visiwani. Alimwona pia kama
dikteta mkimya, asiyeweza kushauriwa akashaurika na watu wa chini
yake.
Nyerere aligundua pia kile pekee kilichomsukuma “ang’are” kwake na kwa
Wabara: kiu ya kurithi nafasi ya Rais baada ya Nyerere.
Baya zaidi lililomuudhi Mwalimu ni kwa Jumbe kugeuka mhafidhina wa
kidini na mpambanaji wa Kiislamu katika Taifa lisilo na dini. Jumbe
alizuru nchi nzima akitoa mihadhara kwenye misikiti hata Serikali
ikalazimika kutoa waraka mkali wa Rais (presidential circular),
kuwakumbusha viongozi wa kitaifa kutojitambulisha na mambo ya kidini.
Hata hivyo, Jumbe alipuuza waraka huo, akaendelea kivyake.
Habari zikamfikia Jumbe juu ya kuanza kupoteza upendeleo wa Nyerere na
kuchuja; zikauma, zikamvunja moyo; uhasama kati ya Jumbe na Nyerere
ukazuka. Katika hali hiyo Muungano ukaanza kutikiswa.
Hatua ya kwanza iliyoanza kutikisa Muungano ilikuwa ni kumrejesha
Tanzania Bara, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Damian Lubuva; badala
yake akamteua raia wa Ghana, Alhaj Bashir K. Swanzy na kumpa uraia.
Kuanzia hapo, madai ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya Katiba,
kupitia mihadhara, magazeti na redio, yalipamba moto. Wengi
watakumbuka matangazo ya redio ya mafichoni, maarufu kama “Kiroboto
tapes”, ya kudai Wazanzibari warejeshewe visiwa vyao, yalivyopamba
moto hadi ilipogunduliwa msituni na wanajeshi kutoka Bara na kuzimwa.
Kwa kupitia Jaji Bashir Swanzy, iliandaliwa hati ya mashtaka kuhoji
muundo na uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalumu ya Kikatiba ya
Jamhuri ya Muungano, ambayo kazi yake pekee, kwa mujibu wa ibara ya
126 ya Katiba ya Muungano ya 1977, “ni kusikiliza shauri lililoletwa
mbele yake na kutoa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na
tafsiri ya Katiba, iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa
kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar”.
Hati hiyo ya mashitaka ilipotea mezani kwa Jumbe katika mazingira ya
kutatanisha, na hatimaye kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere.
Taarifa za uhakika zinaonyesha kuwa waliofanikisha kazi hiyo ni pamoja
na wakubwa wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wakati ule wakiwa
SMZ.
Haraka haraka na hima, kikaitishwa kikao cha NEC ya CCM mjini Dodoma,
Januari 1984 na Jumbe akawekwa kiti moto kwa dhambi ya kujaribu kutua
mahali malaika wanapopaogopa kutua, kwa maana ya kuhoji Muungano;
kisha ikatangazwa “kuchafuka kwa hali ya siasa Zanzibar”.
Bila kumeza maneno, Jumbe alikiri kuandaa hati hiyo kama moja ya haki
zake za kikatiba.
Mbali na hati ya mashitaka, Jumbe aliandaa pia barua ndefu kumkumbusha
Nyerere jinsi Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano zilivyokuwa
zikikiukwa. Alihoji pamoja na mambo mengine, mantiki ya kuunganishwa
kwa TANU na ASP kuunda CCM na mamlaka chama hicho kiliyojipa, ya
kutunga Katiba ya kudumu ya 1977.
Kwa msaada wa Mwanasheria Mkuu Swanzy, Jumbe alifanya rejea Sheria ya
kuahirisha na kusogeza mbele muda wa kuitisha Bunge la Katiba, Namba
18 ya 1965, Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya 1965, na ubatili
wa Katiba ya kudumu ya 1977 kwa namna ilivyobuniwa na kutungwa.
Kwa kuwa barua hiyo ndefu ilikuwa imeandikwa kwa lugha ya Kiingereza,
alimtaka Waziri Kiongozi, Ramadhan Haji, ahakikishe imetafsiriwa kwa
Kiswahili iweze kujadiliwa na Baraza la Mapinduzi.
Kama ilivyotokea kwa hati ya mashitaka, barua hiyo nayo ilitoweka
mezani kwa Jumbe katika mazingira ya kutatanisha na kumfikia Nyerere.
Kwa kuwa alikuwa hajaitia sahihi ilibidi kikao cha NEC kimtake Jumbe
aseme kama hayo ndiyo yalikuwa mawazo yake; naye kwa mara nyingine, na
bila ya kutafuna maneno, alikiri, na hivyo mvua ya mawe ikazidi
kumnyea.
Awali, Januari 12, 1984, Jumbe alihutubia wananchi kwenye kilele cha
sherehe za Mapinduzi, siku chache tu kabla ya kuitwa Dodoma. Katika
hotuba hiyo, hakuficha kukerwa kwa Serikali yake namna Muungano
ulivyotekelezwa kinyume na matakwa asilia. Aliwataka wananchi wawe
wavumilivu na wenye subira wakati tatizo hili likiendelea
kushughulikiwa.
Bila kumeza maneno, na Mwalimu Nyerere akisikia; Jumbe alisema, kama
pasingepatikana mwafaka na maridhiano kati ya Zanzibar na Serikali ya
Muungano juu ya jambo hilo, angelipeleka kwenye Mahakama Maalumu ya
Katiba kupata ufumbuzi kwa yote haya.
Katika kikao cha NEC cha Dodoma, Jumbe alielezewa kama “kiongozi
dhaifu na msaliti wa Muungano”. Alipinduliwa sawia na kupoteza nafasi
zote, kisha akasindikizwa nyumbani kwake na kuwekwa chini ya ulinzi
wakati harakati za kusafisha hewa ya kisiasa zikiendelea.
Tetemeko likawakumba wasaidizi wake wakuu, wakiwamo Waziri Kiongozi,
Ramadhan Haji, Waziri wa Nchi, Aboud Talib, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali mstaafu, Wolfango Dourado wakati Swanzy alirejeshwa kwao
Ghana.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ulinzi wa Muungano na Mjumbe wa NEC, Kanali
Seif Bakari, alipigana kiume kikaoni kujaribu kumwokoa Jumbe, lakini
aliishia kuwekwa chini ya ulinzi wa nyumba yake na hatimaye kizuizini
Tanzania Bara.
Nafasi ya Jumbe ilichukuliwa na Alhaj Ali Hassan Mwinyi, na Seif
Sharrif Hamad akaukwaa Uwaziri Kiongozi.
Je, hayo yalikuwa Mapinduzi dhidi ya Jumbe, kutekwa nyara au zilikuwa
hatua za kinidhamu za chama?.

Jumbe alikuwa Rais wa “nchi” ya Zanzibar kwa mujibu na kwa misingi ya
Katiba ya Zanzibar ya 1979. Na kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano
[Articles of Union] wa 1964, ambao ndio unaosimamia na kutawala Katiba
zote mbili – Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar, suala la Vyama
vya Siasa halikuwa, halijawa na halipashwi kuwa jambo la Muungano.

Kwa mantiki hii, kitendo cha chama cha siasa kumwondoa madarakani Rais
wa “nchi” yenye Katiba yake, yenye Serikali yake na Bunge
lisilotawaliwa na Katiba ya Muungano, ni dhahiri kilikuwa kimevuka
mipaka ya uwezo wake. Kwa sababu hii, hayo yalikuwa Mapinduzi ya
kutumia nguvu ya kisiasa).

Baada ya kazi ya kumpindua Jumbe kukamilika, na ili kuhakikisha
“vituko” vya kuhoji Muungano vimedhibitiwa Visiwani, suala la Usalama
wa Taifa, ambalo kabla ya hapo halikuwa jambo la Muungano (ilikuwa ni
Ulinzi tu), liliingizwa kwenye Muungano kusomeka “Ulinzi na Usalama”.
Kitendo cha Mwalimu Nyerere cha kusimamia na kufanikisha mapinduzi
dhidi ya Jumbe kupitia NEC ya CCM, chama pekee kilichoshika hatamu za
uongozi wa nchi; na kitendo cha kutiwa kizuizini kwa Kanali Seif
Bakari, si tu kilichochea chuki miongoni mwa Wazanzibari kwa Muungano,
bali pia kilizua mgawanyiko wa makundi mawili miongoni mwa viongozi
waandamizi Visiwani na hatimaye kuenea Bara.
Kundi moja ambalo halikufurahishwa na kupinduliwa kwa Jumbe na ambalo
lilitaka kudumisha mapinduzi na fikra za Karume lilijiita
“Wakombozi” (Liberators), na la pili lililotaka mabadiliko haraka na
Zanzibar mpya, lilijiita “Wanamstari wa mbele” (Frontliners). Makundi
haya yalipogongana, moto uliwaka kwa kishindo cha radi.

Kundi la “Wakombozi”, huku limesheheni chuki na hasira ya kulipa
kisasi kwa Nyerere, lilisubiri nafasi na wakati mwafaka kwa tukio zito
kutokea ili limpe kibano na kumdhalilisha, yeye na Muungano kwa
ujumla. Jambo zito hilo lilikuwa nini? Je, kundi hilo liliweza
kutekeleza azima yake?

Na Joseph Mihangwa, Raia Mwema no.226, Tarehe 15 February 2012.

No comments :

Post a Comment