dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, October 28, 2012

TAMKO LA WAISLAMU : KUHUSU KUJIUNGA NA OIC NA KUREJESHWA KWA MAHAKAMA ZA KADHI

BARAZA KUU LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU TANZANIA

TAMKO LA WAISLAMU TANZANIA

KUHUSU KADHIA YA TANZANIA KUJIUNGA NA OIC NA KUREJESHWA KWA MAHAKAMA ZA KADHI

BARAZA KUU LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU TANZANIA

I. UTANGULIZI

Tanzania inapita katika kipindi cha mivutano mikubwa kati ya Waislamu kwa upande mmoja, na serikali na Wakiristo kwa upande mwingine.

Tafauti hizo ni juu ya uhalalali wa urejeshwaji wa Taasisi ya Waislamu ya Mahakama za Kadhi na mchakato wa Tanzania kujiunga na Jumuiya ya misaada ya Waislamu duniani Organization of the Islamic Conference OIC.
Historia inaonesha kuwa kufutwa kwa Mahakama ya Kadhi mwaka 1963 kunatokana na maamuzi ya Bunge kupitia The Magistrates Courts Act, 1963.

Suala jingine ni uhalali na ubora kwa Jamuhuri ya muungano wa Tanganyika na Zanzibari (Tanzania) kujiunga na Shirika la misaada la Waislamu duniani OIC. 
Kutokana na madai ya muda mrefu ya Waislamu ya kutaka kurejeshwa Mahakama ya Kadhi nchini, Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lilitoa jukumu kwa Kamati ya Katiba na Sheria kushughulikia suala hilo chini ya uongozi wa Muheshimiwa Arcado Ntagazwa mwaka 1994. Mwaka 2004 kamati iliendelea na jukumu hilo chini ya uongozi wa Muheshimiwa Athumani Janguo.

Suala hili pia lilijitokeza katika Ilani ya Chama tawala CCM kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2005.

Kamati hiyo chini ya uongozi wa awamu zote mbili ilikutana na Jumuiya za Kiislamu kwa uelewa halisi wa suala husika na vilevile wadau wengine kwa faida za kiutendaji.

Taarifa tulizonazo ni kwamba waraka wa kamati hiyo uliwasilishwa kwa Spika wa Bunge (wa wakati huo) Mh. Pius Msekwa.

Novemba 11, 2007 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia katika hafla ya ‘kusimikwa’ Askofu mkuu wa Kanisa la KKKT Alex Malasusa aliwataarifu watanzania kuwa mapitio ya vyombo husika juu suala la Mahakama ya
Kadhi yamekamilika, akaongeza kuwa wananchi watapatiwa jawabu ya suala hili Februari mwakani, yaani 2008.

Tokea mchakato wa suala hili uanze, na mpaka Rais Kikwete alipotoa tarehe ya kutoa jawabu katika hafla iliyotajwa hapo juu, ni zaidi ya miaka 13 sasa.  Aidha, suala la OIC nalo limepewa urasimu wa aina yake.

Mwaka 1993 Zanzibar ambayo ni moja ya nchi zilizounda serikali ya muungano inayoitwa Tanzania, iliamua kujiunga na OIC kama Zanzibar.  Tanzania bara ilipinga kwa hoja kuwa ni vema ufanyike utafiti wa kina ili maamuzi ya kujiunga au kutojiunga yawe ya pamoja.

Baada ya utafiti wa miaka 15 serikali ya Tanzania kupitia Waziri wake wa mambo ya nje imetamka hadharani kuridhika kwake na sababu zote za kujiunga OIC zikiwemo za kisheria na kiusalama.

Nchi ambazo kwa muda mrefu raia wake wamekuwa wakifaidika kwa misaada ya OIC ni pamoja na Benin, Cameroon, Cote d’Ivoire,  Gabon, Guinea, Guinea Bissau, Msumbiji, Nigeria, Sierra leone, Uganda, Urusi. Nchi hizi ni sehemu ya nchi 57 wanachama wa OIC zikiwemo zenye idadi kubwa ya raia Wakiristo.

Tarehe 24 Oktoba 2008 Maaskofu Tanzania walitoa tamko kali kupinga Mahakama ya Kadhi na OIC. Wameionya serikali kuwa endapo itaridhia kurejeshwa kwa Mahakama ya Kadhi na nchi kujiunga na OIC, mahusiano kati ya Wakristo na Waislamu yatavunjika na uwezekano mkubwa wa kutokea umwagikaji wa damu.

Katika masuala haya, Waislamu wameendelea kusimama kwenye rejea za Sheria, Sharia, Mantiki na Historia. Wakristo wameendelea kusimama katika wasiwasi wa kuwepo kwa itikadi yao na madai ya ‘uvunjwaji wa katiba’ ya nchi. Serikali inaendelea kusuasua katika ahadi za muda mrefu na sura isiyoeleweka.

Waraka huu ambao unakamilika kwa Tamko la Waislamu, unapitia hoja zote tegemezi kwa Wakiristo, Waislamu na mtazamo wa sheria za nchi ili kuitanabahisha serikali itekeleze ahadi zote kama ilivyoahidi, kwa maslahi ya wananchi wote.

II. HOJA ZA MAASKOFU

1. Udini


Miongoni mwa hoja za Maaskofu ni kuwa suala la Kadhi kutambuliwa na katiba ya nchi ni kuleta udini miongoni mwa watanzania. Rejea gazeti la Msema Kweli, na. 578 Jumapili, Septemba 28–Oktoba, 2008, uk. 5.

‘Akitoa tamko hilo Jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Maaskofu wa Kipentekoste nchini, Mwenyekiti wa PCT mkoani hapa Askofu David Mwasota alisema katika awamu nne za uongozi wa nchi, kumekuwapo na juhudi za makusudi kwa baadhi ya viongozi wa serikali, Wabunge na Viongozi wa Dini ya Kiislamu kujaribu kushinikiza udini.’

‘Aliutaja udini huo kuwa ni kutaka kuiingiza Mahakama ya Kadhi ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na pia Tanzania kujiunga na OIC.’

2. Ukiukwaji wa Katiba

Ukiukwaji wa katiba ni moja ya madai ya Maaskofu katika kupinga kurejeshwa kwa Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na OIC. Rejea gazeti la Jibu la Maisha, na.37, Jumapili, Septemba 28 Oktoba 4, 2008, uk. 2.

‘Na wala hatutaki kabisa kuona kinaingizwa kipengele cha kuwa na Mahakama ya Kadhi ndani ya Katiba, maana kwa kufanya hivyo ni kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 toleo la Novemba 1, 2000, Sehemu ya Pili Ibara ya 9 kifungu ‘a’ na Ibara ya 20 (2) a. Kukiuka vifungu hivyo, kutasababisha uvunjifu wa amani na kubomoa mihimili mikuu ya utulivu iliyosimamishwa ndani ya nchi yetu.’

3. Uvunjifu wa Amani

Maaskofu pia wametowa hoja ya uvunjifu wa amani, rejea gazeti la Utatu, Na 044, Jumapili, Septemba 28 - Okotoba 4, 2008 uk. 5.

‘Kwa kuwa Katiba ya nchi yetu hairuhusu serikali ya kidini hatujui linalotafutwa ni nini hasa na serikali kuendelea kuachilia jambo kurudia rudia bungeni, inaashiria nini, hata kama jambo limekubaliwa na chama tawala katika ilani yake, lakini suala hili si la kichama, bali ni la kitaifa na halina maslahi kitaifa maana lina malengo ya kuwagawa Watanzania kidini, hivyo kuchafua amani tunayojivunia muda mrefu.’

4. Kunajisi Katiba

Maaskofu pia wamefika mbali zaidi kwa kutowa hoja kuwa kuingizwa OIC na Mahakama ya Kadhi ni kunajisi katiba ya nchi. Rejea gazeti la Utatu – Na 044, Jumapili, Septemba 28 – Oktoba 4, 2008, uk. 5.

‘Akionyesha wazi msimamo usioyumba wa baraza hilo, Mwenyekiti wa PCT, Dar es Salaam, Askofu David Mwasota aliwaambia waandishi wa habari kuwa uvumilivu wa Wakristo umefikia mwisho na sasa wanasema hapana, hawataki Katiba ya nchi itiwe unajisi na sheria za dini.'

Aidha, kwenye Tahariri ya gazeti hilo Uk. 4. imeeleza kama ifuatavyo.

‘Tusikubali kutia unajisi katiba ya nchi, iachwe ikibaki kama katiba na dini zetu zibaki kama zilivyo, kwani kucheza na eneo hilo ni kuchezea aliyeumba mbingu na nchi ambaye ana mamlaka juu ya yeyote na chochote.’

5. Kujitafutia laana ya Biblia, Tanzania

Imeelezwa kuwa ‘Yabainika Tanzania kujiunga na OIC ni kujitafutia laana ya biblia.’ Rejea gazeti la Msema Kweli Na. 579 Jumapili, Oktoba 5-11, 2008, Ukurasa wa mbele na Uk. 5,

‘Imebainika kuwa malengo ya Shirika la Umoja wa Kiislamu (OIC) yatailetea laana kubwa Tanzania iwapo itajiunga nalo, kutokana na moja ya malengo yake kupinga uwepo wa taifa la Kiyahudi la Israeli katika eneo la Mashariki ya Kati, huku tayari Biblia Tukufu ikiwa imetahadharisha kuwa yeyote atakayekwenda kinyume na taifa hilo atakuwa amejipatia laana.’

‘Ukweli wa laana ambayo Tanzania itajipatia ikiwa itajiunga na OIC inaelezwa vyema katika Biblia kwenye Kitabu cha Mwanzo 12:3 ambapo baada ya Mungu kumwahidi baraka kuu Nabii Abrahamu ambaye ni chimbuko la taifa la Israeli, alisisitiza ahadi zake kwa kuweka Agano kwamba atawabariki wote watakaombariki na kuwalaani wote watakaomlaani.’

6. Kuisilimisha nchi

Rejea gazeti la Msema Kweli - Na. 578, Jumapili, Septemba 28 Oktoba 4, 2008, Ukurasa wa mbele na Uk 5, chini ya kichwa cha habari:

‘Katiba ya OIC kuibadilisha Tanzania kuwa dola ya kiislamu.’

‘Juhudi zinazoendelea hivi sasa za kutaka Tanzania ijiunge na Shirika la Umoja wa Kiislamu maarufu kama Organization of the Islamic Conference (OIC), huenda zikaigeuza kuwa dola la Kiislamu kutokana na katiba ya Shirika hilo kueleza kuwa sifa ya kujiunga nalo ni nchi au dola husika kuwa la Kiislamu.’

‘Hiyo inamaanisha kuwa ikiwa Tanzania ina nia ya kujiunga na OIC ni lazima kwanza iwe dola la Kiislamu na ndipo ipate ridhaa hiyo.’

7.   Wakristo hawakubali kuhukumiwa na Qur’an.

Rejea gazeti la Msema Kweli Na. 579, Jumapili, Oktoba 5–11, 2008, Uk. 3.

‘Nchi yetu ni ya amani na upendo kwa miaka mingi, hivyo endapo wataiweka mahakama hiyo ndani ya katiba ni kutafuta kuingiza dini fulani kwenye nchi na kufanya hivyo ni chanzo cha mafarakano kwani Mkristo hawezi kuhukumiwa na Qur’an.’

8. Kutumia Siasa

Wakristo watishia kutumia karata ya siasa kukataa kuja kwa OIC na mahakama ya kadhi. Rejea gazeti la msema kweli Na. 579 Jumapili, Oktoba 5 – 11, 2008, Uk. 3.

‘Mchungaji wa Kanisa la Glory of Christ lililopo Ubungo Kibo Jijini Dar es Salaam, Josephat Gwajima, ameitaka serikali kubadilisha uamuzi wake wa kuiweka Mahakama ya Kadhi katika Katiba ya nchi pamoja na kujiunga na umoja wa nchi za Kiislamu duniani (OIC) na endapo itafanya hivyo, Wakristo hawatakuwa tayari kukipigia kura chama chenye mambo hayo kwenye Katiba zake, wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao.’

Pia rejea gazeti Nyakati Na.408, Jumapili, Septemba 28, Oktoba 4, 2008–Uk. 7.

‘Sisi kama Wakristo tunalichukulia jambo hili kuwa ni la kisiasa zaidi kuliko la kitaifa na tunajua hatari yake kijamii, hata kama Waislamu wanavyolazimisha kwamba haitawahusu WAKRISTO. Hivyo ikibidi kuwatahadharisha waumini wetu kuwa waangalifu kwa, vyama vya siasa vyenye sera na ilani zenye hatari kama hizi inapofika nyakati za uchaguzi waone hatari zilizoko mbele kitaifa. Itakuwa haki kwetu mbele za Mungu, mbele ya dunia, kikatiba na kama mwasisi wa taifa hili alivyoona mbali akitutaka raia wote wa Tanzania tukumbatie suala la kutoingiza mambo ya dini ndani ya Katiba na Serikali’

Mbali na kauli hizi za makundi tofauti ya kikristo, walitowa tamko la pamoja kupinga chini ya PCT na chombo kikuu kinachowaunganisha Baraza la Maaskofu, CCT. Rejea gazeti la Nyakati Na. 408 Jumapili, Septemba 28 –Oktoba 4, 2008, uk. 6.

‘Kwa mujibu wa Askofu Mwasota, wakati tamko lao lilipokuwa likitolewa mapema Jumanne, iliyopita, harakati mbalimbali za kupinga azimio lililotangazwa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Benard Membe, la Tanzania kujiunga na OIC akisema itafaidika kiuchumi na kijamii, zilikuwa zinaandaliwa.’

‘Habari zaidi zinaeleza kwamba PCT mkoa wa Dar es Salaam, ni kundi tangulizi tu lililojitokeza lakini msimamo wao ndio ule ule wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ambao walishatoa kauli zao kwa mitindo tofauti kupinga swali hilo’.

III. MAKINZANO YA HOJA ZA MAASKOFU NA REJEA ZA KITAIFA NA    KIMATAIFA.

1. Kujiunga na OIC hakuifanyi Tanzania kuwa nchi ya Kiislamu

Kujiunga na OIC hakuifanyi Tanzania kuwa nchi ya Kiislamu kama Maaskofu wanavyotaka ieleweke. OIC ina nchi wanachama wa aina mbili:

a) Nchi ambazo Katiba zao zinatamka wazi kuwa serikali zao ni za      kisekula (hazina dini). Miongoni mwa hizo ni Albania,  Benin, Burkina
Faso, Cameroon, Cote d’Ivoire,  Gabon, Gambia,  Guinea, Guinea Bissau, Guyana,  Lebanon,  Msumbiji, Niger, Nigeria, Senegal,  Sierra leone, Uganda, Urusi, Uturuki,

b)  Nchi ambazo Katiba zao zinatamka wazi kuwa ni nchi za kiislamu au      Uislamu ndiyo dini rasmi ya Taifa lao. Mfano Indonesia,  Iran,
     Malaysia, Misri, Pakistan, Turkimenistan, Saudia, Sudan na      nyenginezo.

Kwa hiyo, si kweli kwamba OIC inakutanisha nchi za Kiislamu tu na au nchi ikijiunga hatimae huwa ni nchi ya Kiislamu. Kama hayo ni kweli, tungeshuhudia nchi kama Cameroon, Msumbiji, na Uganda ambazo ni wanachama wa OIC kulazimishwa kuwa nchi za kiislamu kama Maaskofu wanavyodai. OIC ni taasisi ya kimataifa ya kiuchumi na kijamii iliyoundwa na waislamu, na nchi kadha zikiwemo zenye raia wengi wakiristo zimenufaika na uanachama huo.

 2. Mahusiano na taasisi za kidini

Sio siri kuwa Tanzania ina uhusiano wa kibalozi na HOLY SEE ambayo ni mamlaka ya kidini yanayo tawalia Dola ya Vatikano.

Tanzania pia imeingia Mkataba wa Maridhiano (Memorandum of Understanding) na Makanisa ya CCT na TEC kwa ushirikiano na Makanisa ya Ujerumani (Germany Churches Partners) tangu mwaka 1992.

Vilevile Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth) ambayo kiongozi wake ni Malkia wa Uingereza ambaye pia ni MKuu wa Kanisa Anglikana duniani.

Kwa rejea hizi utaona wazi kuwa dhana ya nchi ya Tanzania kuingizwa katika udini na uvunjaji wa katiba inakuja pale tu mikataba ya kitaifa na kimataifa inapo tamka neno uislamu.

Hatuwezi kuukataa ukweli kwamba OIC ni Umoja wa nchi za waislamu kama Charter ya mkusanyiko huu inavyoonyesha. Malengo mengine ya OIC ni ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kuliko kidini na ndiyo maana hata nchi zisizokuwa za kiislamu Gabon, Cameroon, Msumbiji, Marekani, Uganda na Urusi- zimejiunga na umoja huo kama wanachama kamili full membership au wanachama watazamaji observer membership ili kupata faida hizo za kiuchumi na kijamii.

Kama ambavyo serikali na wakiristo walivyoona si kinyume na katiba Tanzania kuwa na uhusiano wa kibalozi na Papa Holy See ama Vatican, basi kwa hoja hiyo hiyo si kinyume na katiba kwa Tanzania kujiunga na OIC.
Kuna tofauti kati ya “The Vatican” na “Holy See”. The Holy See ni mamlaka inayoitawala Vatican. Mamlaka hiyo ina madaraka kamili (sovereignity entity) yanayoongozwa na Papa na huwakilisha Kanisa Katoliki katika masuala ya kidunia.

Aidha, kwa mujibu wa tovuti ya ‘Holy See’, wanasema ifuatavyo:

‘The Holy See should not be confused with The Vatican City State which came into existence only in 1929 while the Holy See dates back to early Christian times. Ambassadors are officially accredited not to the Vatican City State but to “the Holy See” and Papal representatives to states and international organizations are recognized as representing the Holy See, not the Vatican City State’.

Mamlaka ya Upapa na Vatican ni vitu viwili tofauti kwa hoja zifuatazo:

Mosi, Vatican ilianzishwa 1929 wakati Holy See ipo toka zama za mwanzo za Ukristo baada ya Mkutano wa Nicaea 325 A.D.

Pili, Holy See ndiyo inayotawala Vatican City State.

Tatu, Mabalozi huchaguliwa na Papa na humuwakilisha Papa na si Vatican.

Nne, Mabalozi wa nchi zenye uhusiano na Holy See huwasilisha hati zao za ubalozi kwa Papa na sio Vatican.

Tano, Lugha rasmi ya Holy See ni Kilatini, wakati ile ya Vatican ni Kiitaliano.

Sita, Hata Pasi za kusafiria za Holy See na Vatican ni tofauti.

Ni vema katika nukta hii ikumbukwe kuwa nchi inapokuwa na uhusiano na Vatican, kimsingi, inakuwa na uhusiano na Papa (mamlaka ya kidini ya Holy See) jambo ambalo kwa mujibu wa Maaskofu hao ni must be avoided at all costs  kwa sababu ni kinyume cha misingi ya kisekula. Kwa mfano katika mwezi wa October 2008, Balozi wa ‘Vatican’ Tanzania, alifanya ziara mkoani Mbeya ianyoitwa ziara ya kiroho kwa mujibu wa vyombo vya habari.

Na kwa kuzingatia ukweli huu, na kama Maaskofu hawa wangekuwa watetezi wa kweli wa Katiba, tungewasikia wakipinga uhusiano wa kibalozi kati ya Tanzania na Mamlaka ya Upapa moja kwa moja au kupitia Vatican, jambo ambalo hivi sasa Tanzania inalazimika kuwa na mabalozi wawili (Balozi wa Tanzania Italia na yule wa Tanzania kwa Holy See) na pia kuna ubalozi mdogo (Consulate) wa Milan katika nchi moja tu ya Italia.

Wakati hayo yakijiri kwa Tanzania kuwa na mabalozi watatu katika nchi ya Italia pekee kutokana na uhusiano wake na Holy See, nchi nyingi duniani zenye umuhimu mkubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa nchi yetu, Tanzania inawakilishwa na balozi mmoja tu,  mfano, nchi za Saudi Arabia, Kuwait na Qatar inawakilishwa na balozi mmoja tu.

Ulazima huu wa kuwa na mabalozi wawili nchini Italia unathibitishwa na maandiko yaliyo katika tovuti ya Holy See www.wikipedia/Holy_See yasemayo;-

“The Holy See (not the State of Vatican City) maintains formal diplomatic relations with 176 sovereign states, the European Union and the Sovereign Military Order of Malta; 69 of the diplomatic missions accredited to the Holy See are situated in Rome, though those countries then have two embassies in the same city, since, by agreement between the Holy See and Italy, the same person cannot be accredited simultaneously to both”. (Ibid; Msisitizo wa kwetu).

Hivi ndivyo walivyoona Maaskofu wenzao nchini Marekani. Katika Makala yake Ambassadors to Vatican: Breaching the Church-State Wall, Mkurugenzi Mtendaji wa Baptists Christian Life Commission huko Nashville Marekani, Richard D. Land alimwandikia barua Rais Mteule wa Marekani wakati huo Bill Clinton akisema hivi:

‘How does the United States, our diverse democracy, justify the deployment of American Ambassador to the Vatican? This is a gross abrogation of church-state separation that relegates all other religions to a lesser status’.

Kisha wakahoji mantiki hiyo kwa kusema ‘Why don’t we send ambassadors to Canterbury, Mecca, Jerusalem-to all other religion headquarters worldwide to difuse the smell of favouratism?)

Wameendelea kusema: How does our government get away with meddling, both at home and abroad, in any religious body at all? Danger! Stop! Why, oh why are we not outraged and howling in protest? Here we sit, year after year, watching our presidents and most of Congress who, greedy for votes, are too chicken to call halt to this’. (Washington Post, December 5, 1992).

Izingatiwe kuwa Marekani haikuwa na Ubalozi wowote Vatican toka 1776 mpaka mwaka 1984 wakati Rais Ronald Reagan alipoanza kutuma mabalozi Vatican.

Maaskofu wa CCT walipaswa kuhoji kwanza kwa nini tuwe na Ubalozi Holy See na Holy See iwe na Ubalozi Tanzania nchi ambayo ni ya kisekula kabla ya kuhoji Tanzania kujiunga na OIC? Lakini pia walitakiwa kuona kuvunjika kwa katiba pale ambapo wao wana uraia wa nchi mbili, Vatikani na Tanzania, jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi. Ajabu iliyoje kwa wenzetu kuwa na hoja kengeza katika hili!  

Kwa Serikali kuendelea kuwa na Ubalozi wa Papa hapa nchini itakuwa na sura mbili, jambo ambalo kama walivyosema Maaskofu wa Marekani tuliowanukuu hapo juu linazidhalilisha dini nyingine na kuonyesha upendeleo wa wazi kwa dini ya Kikatoliki dhidi ya waislamu, bali hata dhidi ya wakristo wasiokuwa  wakatoliki.

Uhusiano wa Tanzania na Papa/Vatican, hauna maslahi ya kitaifa katika uchumi wala kijamii ukilinganisha  na historia ya OIC na nchi wanachama wake. Pengine hiyo ndio picha ambayo Maaskofu wa Tanzania wasingependa ijulikane. Pia, wana hofu jamii nyengine kupata nguvu zenye maslahi kupitia OIC kama wao walivyopata nguvu kubwa kupitia mkataba uliopo baina yao na serikali Memorandum of Understanding.

3. Wakiristo wanavyonufaika na Memorandum of Understanding.

Katika Makala “The Tanzania Catholic Church” iliyo katika tovuti ya Kanisa Katoliki (www.rc.net/tanzania)-tovuti ambayo iko chini ya Askofu Method Kilaini, panazungumziwa faida wanazopata wakristo peke yao kutokana na Memorandum of Understanding kama ifuatavyo:

‘To strengthen their social services sector, the two Church bodies that is the Protestants under Christian Council of Tanzania (CCT) and the Catholics under the Tanzania Episcopal Conference (TEC), in 1992 assisted by the German partner Churches negotiated a
‘Memorandum of Understanding” with the Tanzania government. In this memorandum, the government recognized the important role played by the Churches in the social sector of the country, pledged to help the Churches by sharing with them grants from foreign government and promised never to nationalize church institution again’.

The ‘Memorandum of Understanding’ authorized the forming of ‘Christian Social Services Commission’ (CSSC). TEC and CCT are each represented by the Secretary and four bishops. The commission has two executive organs, the Christian Medical Board of Tanzania (CMBT) and the Christian Educational Board of Tanzania (CEBT) for health and education respectively.

This commission formulates common policies for the Education and medical services of the Churches and negotiate with the Tanzania government in the name of the Churches. The two executive organs run common programs. The churches together run more than 50% of the Medical Services and secondary schools in the country’.

Kanisa kupokea sehemu ya pato la taifa na kuliacha kundi jingine la dini katika hali duni kiuchumi, kijamii na kielimu, je huku si udini kuvunja Katiba? Mbona waliosaini makubaliano haya hawakuhisi kama hali hiyo inaweza kuvuruga mshikamano wa kitaifa kama ambavyo wanavyodai katika suala la Kadhi na OIC.

Bila shaka Maaskofu hawana hoja bali wana chuki dhidi ya Uislamu, (Islamaphobia), kiasi cha kutoona boriti lililo katika jicho lao bali wanaona kibanzi kilikicho katika jicho la wengine.

IV. MAHAKAMA YA KADHI NA ULIMWENGU WA KISEKULA

Moja ya kadhia inayo athiri ustawi wa jamii ya Waislamu nchini Tanzania hivi leo ni kuondolewa Mahakama za makadhi, ambazo mahakimu na majaji ni wafasiri tu wa sharia (dispensers of law).

Kwa waislamu, kuhukumiwa kwa sheria ya Allah (sw) ni sehemu ya imani yao. Sheria za kiislamu zilikuwepo kabla ya katiba zinazotawalia nchi mbalimbali hivi sasa.

‘Na ndivyo hivyo tumekuweka juu ya sheria katika kila jambo, basi ifuate na wala usifuate matamanio yao yakaja yakakutoa katika njia (dini) ya mola wako’. (48:45)

‘Na wale wasiohukumu kwa aliyoyateremsha M/Mungu, basi hao ndio makafiri… Madhwaalimu… Mafaasiq’ (5: 44-47).

Uislamu ni dini ya Allah Ambaye Habadiliki. Sharia zake hazitungwi na Mitume, wala watu wa kawaida, na hazibadilishwi, kufutwa kuongezwa na wala kupunguzwa. Waislamu watakapoishi pasina kutekeleza sheria za Mwenyezi Mungu watakuwa wametoka katika misingi ya imani yao. Na ili sheria za kiislamu zitumike katika jamii yao ni lazima pawepo mahakama za makadhi. Ili suala hili lieleweke, ni vema nukta zifuatazo zikazingatiwa:

1. KADHI NI NANI KISHERIA?

Kadhi kisheria ni ‘yule anayehukumu kwa kutumia sharia’. Hii ni kutokana na neno la kiarabu ‘Qadhwaa’ ambalo lina maana ‘Hukumu’. Utaratibu wa kuwa na “kadhi” pia umeelekezwa katika Biblia  (Taz. Mathayo 5:25-27 na pia Ezra na Matendo ya Mitume)
2. HISTORIA YA MAHAKAMA ZA MAKADHI.

2.1         Zama za Mtume (saw).

Wakati wa uhai wa Mtume (SAW) hapakuwa na Makadhi. Hii ni kwa sababu Mtume (SAW) mwenyewe alikuwa ndiye Kadhi. Alikuwa akihukumu kesi za aina zote kwani ndio moja ya malengo ya kutumwa kwa walimwengu:

‘Basi naapa kwa jina la Mola wako hawawezi kuwa waumini (wakweli) mpaka wakufanye Hakimu katika yale wanayo khitilafiana baina yao kisha wasipate uzito katika hukumu utakazohukumu’ (4 :65)

2.2           Zama za Makhalifa Waongofu.

Katika zama za Makhalifa Waongofu; (yaani Waliongoza Uislamu baada ya Mtume Muhammad saw) Abubakar, Umar, Uthman na Ali (r.a) waliteuliwa watu waadilifu wenye kuielewa vema Qur’ani na Sunnah ya Mtume (saw) wakawa wakihukumu watu kwa sheria ya Allah, hawa waliitwa Makadhi.

Miongoni mwao ni; Al alama Iyaadh ambaye alitoa ile hukumu maarufu dhidi ya Khalifa wa nne Ali Bin Abii Twaalib (r.a) kwa kumpa ushindi Myahudi baada ya Ali (r.a) kukosa ushahidi wa kutosheleza katika kesi ya kupotelewa na ngao.

Kipindi cha Mtume (saw) na wakati wa Makhalifa, Misikiti ilibeba dhima ya majengo ya mahakama za Kadhi. Hukumu zote zilitolewa msikitini.

Makadhi walihukumu kwa Sharia hawakumuogopa yeyote isipokuwa Allah. walijua hata kama wameteuliwa na mtawala lakini wao wanawajibika kwa Allah. Mtawala (Khalifa) alipotuhumiwa alisimamishwa mbele ya Kadhi.

2.3           Baada ya Makhalifa Waongofu.

Kipindi hiki kilianza na dola ya Banuu Umayyah na kufuatiwa na Banuu Abbas na dola za wafalme wengine zilizokuja baadaye.

Katika kipindi hiki mfumo wa Mahakama za Makadhi uliingia katika kipindi cha tatu cha ukuaji wake. Majengo maalumu ya mahakama yalijengwa, uratibu na udhibiti wa mashauri kwa mujibu wa uzito wake uliendelea kuzingatiwa.

2.4           Zama za Ukoloni.

Kimsingi, Ukoloni ulikuja na agenda dhidi ya Uislamu. Agenda waliyokuja nayo ni Ukristo kama Historia inavyothibitisha jambo hili: Katika mkutano uliofanyika Berlin kuligawa bara la Afrika - maarufu “The Berlin Conference of 1884-85”, wakoloni walikubaliana kuulinda ukristo. Kipengele kimojawapo katika makubaliano ya Berlin kinasema;-
“Christian missionaries, scientists, and explorers, with their followers, property, and collections, shall likewise be the objects of especial protection”. (http://en.wikipedia.org/wiki/Berlin_Conference)

‘The Christian missionary works paved the way for eventual colonization of Africa’ (Walter Rodney - How Europe Underdeveloped Africa).

Kwa hiyo, wakoloni ingawa walionekana kwa nje kuwa wasekula, mataifa yote ya kikoloni yalijiita “Christian Powers” - Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji, Ureno, Hispania na Italia. Hata ilipoundwa League of Nations (mtangulizi wa UN) jina lake rasmi lilikuwa “The League of Nations of Christian Powers”. Mpaka leo mataifa haya bado yanajivunia Christian heritage.

Kwa hiyo wote waliapa kupigana vita vya msalaba (Crusade) dhidi ya uislamu wakiuona uislamu kuwa ni adui mkubwa anayepaswa kupigwa vita na kuangushwa kupitia mifumo mbali mbali. Kwa maneno yake Mwanahistoria maarufu, W.W. Hunter (1871) anasema kuwa:

‘the Mussalmans are in all aspects a race ruined under the British Rule’

‘Mohammedan element in India is that which causes us most trouble and provokes the largest share of our hostility. Our antagonism to the followers of Mohamed is far stronger that that between us and the worshippers of Shiva and Veshnu. They (muslims) are unquestionable more dangerous to our rule” (W.H.Russel, My Diary in India, Vol.II, pp 73-74, London, 1890).

Kilele cha chuki za Wakoloni Wakristo dhidi ya waislamu kinadhihirika pale Waziri Mkuu wa Uingereza Palmerston (aliyeishi tangu 1784-1865) alipomwamuru Gavana Mkuu wa India Lord Canning, ahakikishe kwamba kila nyumba ya muislamu nchini India inavunjwa.

‘Raze to the ground every building belonging to Muslims without regard to antiquarian veneration or artistic predilection’ (W.W. Hunter, Indian Mussalmans, Are They Bound in Conscience To Rebel Against The Queen, p.31, Calcuta (1871)).

Maana yake:

‘Bomoa kila jingo linalimilikiwa na Muislamu bila kujali thamani yake kwa ukale wake au mvuto wake wa kisanaa’


2.5. HISTORIA YA MAHAKAMA ZA MAKADHI TANZANIA.

2.5.1. Kuingia kwa Wareno (Wakatoliki):

Mahakama za makadhi Afrika ya Mashariki zilikuwapo tangu uhai wa utawala wa Makhalifa waongofu wanne. Wareno walipovamia Afrika ya Mashariki, Waliwakuta waislamu wakitumia sharia zao ikiwemo Mahakama ya Kadhi. Ingawa walifanya njama nyingi za kufisidi Uislamu, waliondoka na kuziwacha Mahakama za Kadhi zikifanya kazi.

2.5.2. Kuja kwa Wajerumani (Walutheri):

Wajerumani walipoingi Afrika mashariki waliwaajiri Waislamu katika mambo ya kiutawala kwa kuwa ndio watu pekee waliokuwa wameelimika na kustaarabika wakati huo, mfumo wa elimu uliokuwapo ulitumia lugha za Kiarabu na Kiswahili.

‘In the early colonial period, the Moslems being the only literate people in the country were used everywhere as sub-officers’ (The Tanzania Catholic Church, www.rc.net/tanzania/tec).

Maana yake:
‘Katika kipindi cha awali cha ukoloni, Waislamu walitumiwa kama makarani kwa kuwa ni wao peke yao ndiyo walikuwa wakijuwa kusoma na kuandika.’

Pia Wajerumani walipoondoka waliacha, mahakama za liwali ambazo zilikuwa ni sehemu ya mahakama za makadhi.

2.5.3. Zama za Waingereza (Waangalikana):

Muingereza alipoingia Afrika ya Mashariki, alileta uzoefu alioupata bara Hindi jinsi ya kuwadhibiti waislamu kama tulivyoona huko nyuma. Alichofanya Muingereza ni kuwatenga Waislamu kutoka katika nafasi zote za utawala na mfumo wa elimu.

Hata hivyo, Muingereza hakutaka kuwakabili Waislamu moja kwa moja kwa sababu walielewa kuwa kufanya hivyo ni hatari. Dr. Ambedkar alipata kunukuliwa akisema:

‘No government can exercise its power in such a manner as to provoke Muslims to raise in rebellion. I think it would be a mad government if it did so.  (Justice V.R Krishna Iyer, Reform of The Muslim Personal Law, Bombay, p.17, 1970)
Maana yake:

Kwa hiyo, Muingereza alipanga kuwadhoofisha waislamu hatua kwa hatua. Kwanza, kielimu, Pili, Kiuchumi na hatimaye Kijamii.

Katika kutekeleza mkakati huo, mfumo wa sheria ulitumika kama tunavyojifunza kutoka India. Mbinu walizoitumia Wakoloni Waingereza ni hizi zifuatazo; Kutunga Katiba na kufanya marekebisho ya katiba mara kwa mara (Constitutional laws and amendments), Mfumo wa mahakama (Judiciary System), Mfumo wa Elimu (Educational System), na  Vyombo vya Habari (The Mass Media). Jaji wa Mahakama Kuu nchini India alipata kusema kuwa;

‘Let us tackle the job of mordenizing the Islamic law…Our Muslim brothers should remember that matters of civil concern do not affect the core of the Prophet’s religious teachings but fall under the great guidance given by Jesus: Render to the Caesar what is due to him and to God what belongs to Him’ (Justice V.R Krishna Iyer, Reform of The Muslim Personal Law, Bombay, p.17, 1970)

Aidha, Jaji V.R Krishna aliongeza akisema kuwa;

‘Silent but substantial reforms through judicial activism is an unexploited field in India because they (the judges) are not militantly committed to the secular mission of the constitution…Uninhibited judicial adventure in open areas of Muslim law can be fruitful’  (The VII Constitutional Assembly Debates (1949), pp 781-82, Calcuta, India).

Hapo ndipo inapothibitika mkakati wa watawala kuhujumu sheria za kiislamu kupitia mfumo wa sheria na mahakama. Mkoloni muingereza Mwaka 1920 akatunga sheria iliyojulikana kama  “The Court Ordinance of 1920”. Katika sheria hii, mfumo wa mahakama ukawa na sehemu tatu; Sheria za Kisekula (The secular (common) laws), Sheria za Kiislamu (The Islamic law), na Sheria za Mila (The Customary law)

Kwa upande wa sheria za kiislamu, mahakama maalum zilizojulikana kama “Mahakama za Liwali” ziliendelea kujengwa mbali na mahakama za serikali. Mabaki ya majengo hayo yapo mpaka leo katika sehemu mbali mbali nchini likiwemo lile lililopo Mjini Musoma. Majengo haya ni kumbukumbu kwamba wakati Fulani Waislamu wa nchi hii walikuwa na hadhi na heshima yao na walikuwa na mfumo wao wa sheria.

Hata hivyo, katika miaka ya hamsini (1950’s), Waingereza walituma tume mbili hivi zikiitwa “The Royal Commission” ili kuangalia namna ya kuziengua sheria za kiislamu hatua kwa hatua kwa kuanzia na kupiga marufuku adhabu kadhaa zilizokuwa zikitolewa na mahakama za kadhi. Tume hizi ziliweka msingi ambao hatimaye ulipelekea kufutwa kwa mamlaka za machifu na mahakama za kadhi.

2. 5. 4. Makahakama za Kadhi Katika Tanganyika huru.

Mahakama za makadhi zilikuwepo hata mara tu bada ya uhuru wa Tanganyika na hazikuleta faraka, ugomvi wala kuvunja umoja wa kitaifa. Bila shaka wakati ambao umoja wa kitaifa ulidhihirika ni wakati wa kudai uhuru ambapo ingawa waislamu ndio walioongoza harakati hizo, lakini waliwapokea wakristo wachache waliojiunga nao kama Mwl Nyerere, John Rupia, Kambona huku wakristo wengi wakichukua msimamo wa Kanisa kutojiingiza katika kudai uhuru. (Reja tovuti ya RC www.rc.net/tanzania/tec).

Lakini mara tu baada ya uhuru kupatikana, mwaka 1963, ikaanzishwa sheria iitwayo ’The Magistrate Court Ordinance of 1963’ kuchukua nafasi ya ile ya mwaka 1920. Sheria hii ndiyo inayodaiwa kuzivunja mahakama za kadhi na za kimila, na hivyo kuwalazimisha Waislamu kufuata sheria zote za kisekula kinyume na dini yao na mila zao jambo ambalo ni kuvunja haki za binadamu kama zilivoaishishwa na tamko la Umoja wa Mataifa (The Universal Declaration of Human Rights) ambalo Tanzania ilikwishalisaini wakati huo.

Tangu mwaka 1963 mpaka sasa ni miaka 45 , mambo ya waislamu, ndoa, mirathi, talaka, amana, wakfu yanaendeshwa na serikali kwa kutumia sheria za kisekula kinyume cha Katiba 19(1) na matakwa ya waislamu.

Sababu zilizoelezwa wakati wa kuondolewa mahakama za makadhi mwaka 1963 zilikuwa ni hizi zifuatazo;
1.                Kuleta usawa, haki na umoja wa kitaifa.
2.                Serikali haikuwa na fedha za kugharamia mahakama za makadhi.
3.                Ilikuwa ni katika maazimio ya vyama kadhaa vya kupigania uhuru barani Afrika (Angalia kabrasha la tume ya kukusanya maoni kuhusu adhabu ya kifo na kurejeshwa kwa mahakama za makadhi)

Sababu hizi si za msingi wakati huo na hata leo, kwa sababu, kama waislamu tungepewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi hayo ya kuondolewa Mahakama za Makadhi mwaka 1963 kama ambavyo wakristo wanashirikishwa katika mchakato wa kurejeshwa mahakama za makadhi hivi sasa tungehoji kama ifuatavyo:

Mosi, kuwepo kwa mahakama za kadhi kungehatarisha haki ipi na kwa vipi ambayo gharama yake ni kuondolewa haki ya msingi ya Waislamu Tanzania?

Pili, Kama kweli serikali haikuwa na fedha za kuendesha mahakama hizo si wangewataka waislamu kuchangia mahakama hizo? Waislamu wangeweza kuwasiliana na wenzao Afrika Mashariki wakati huo wanayo EAMWS au kwingineko duniani kupata fedha hizo au kuchangia kwa njia ya sadaka, zaka, wakfu kama walivyokuwa wakiziendesha kabla ya kuja wakoloni.

N.B: Na hata sasa inatolewa hoja hii kwamba kama mahakama za kadhi zitarejeshwa, fedha za kuendesha mahakama hizo zinatoka wapi? Sisi twasema fedha zitatoka serikalini kwani serikali inapata wapi fedha za kuendesha mashule, mahospitali na taasisi za kikristo kupitia Hati ya Maridhiano kati ya Serikali na Makanisa (Memorandum of Undertanding)?

Tatu, Maazimio ya vyama vya kupigania uhuru yalihalalishaje kuondolewa kwa mahakama za makadhi? Vipi uhuru utafutwe kwa kuondoa uhuru wa ibada kwa waislamu?

2.5.5. Kuwepo kwa Mahakama za Makadhi si Kuvunja Katiba

Hoja kuwa kurejeshwa kwa mahakama za makadhi kutavunja katiba ya nchi haina mantiki yoyote. Sababu yake ni kuwa katiba hiyo hiyo imewapa wananchi wote uhuru wa kuabudu na kufuata dini wazitakazo. Katiba imefanya hivi huku ikifahamika kuwa masuala ya namna ya kuoa, kuachana katika ndoa, kurithisha, kutoa sadaka na kuweka mali wakfu, kulea watoto, na masuala ya kifamilia kwa ujumla wake kimsingi ni mambo ya kiibada kwa kuwa yanafungamana moja kwa moja na dini na imani ya mtu husika. Ruhusa na uhuru huu wa kuabudu na kuamini dini kila mmoja anayoipenda ndiko kuliko pelekea ruhusa ya kutumika kwa sheria za dini na mila katika masuala haya.

Ni jambo la kimantiki kuwa iwapo sheria fulani imeruhusiwa kutumika, basi na mahakama zifaazo kuamua masuala yahusuyo sheria hiyo pia ziwepo. Kwani itakuwa haina maana kuwa na sheria ambayo haina mahakama zifaazo kuamua migogoro ihusuyo sheria hiyo. 
Hali kama hiyo itaifanya sheria hiyo ikose maana, heshima na mwishowe itapuuzwa nakuacha kufuatwa.

Paragrafu ya pili ya proviso ya fungu la 11(1) la Judicature and Application of Laws Act, Sura ya 358, Mapitio ya mwaka 2002 inaeleza kuwa sheria ya kiislamu itatumika katika masuala ya ndoa, talaka, usimamizi wa watoto, mirathi, wakf na masuala kama haya kwa watu wa jamii inayofuata sheria hiyo – yaani, waislamu.

Hakuna yeyote aliyepata kusema kuwa fungu hili la sheria linavunja katiba ya nchi. Kinyume chake ni kuwa fungu hili la sheria halivunji katiba bali linaikamilisha kwa kuwapa haki waislamu kufuata taratibu za dini yao katika masuala haya ya kiibada kama walivyorususiwa na katiba kuamini na kuabudu kwa mujibu wa dini yao. Kutaka iwe kinyume na hivi ni kutaka kuvunja katiba kwa kuwazuia waislamu kutekeleza mambo haya ya kiibada kwa uhuru.

Kama tulivyotangulia kusema, hakutakuwa na maana kuweka sheria bila kuweka mahakama zinazofaa. La kujiuliza hapa ni je, mahakama zilizoko kweli zinafaa kusimamia utoaji maamuzi katika masuala yahusuyo sheria ya kiislamu hapa nchini?

Jawabu la swali hili ni hapana iliyo bayana. Kwa uchache, sababu zifuatazo zinatosheleza kuonyesha kuwa mahakama hizi hazifai:-

Mosi, Kwa mujibu wa imani ya kiislamu, asiye muislamu hapaswi kuhukumu kwa sheria ya kiislamu kwa sababu sheria hizo ni imani ya waislamu kama ambavyo hapaswi kufunga Ramadhani, kusali sala tano, kuhiji Makka na mengineyo yaliyo ya dini ya kiislamu.

Pili, hakimu au jaji asiyekuwa muislamu hawezi kutenda haki kwa muislamu kwa sababu hakimu au jaji anatakiwa siyo tu kutumia sheria kuhukumu bali aiamini sheria hiyo moyoni mwake vinginevyo anakuwa katika hali ya kisaikolojia ambayo haifai kutoa hukumu kwa sheria husika.

Tatu, mwenye kuhukumiwa naye si tu ahukumiwe bali anatakiwa awe na imani na sheria inayotumika kumhukumu, mahakama na hakimu au/na jaji anayemhukumu. Ndiyo maana mtuhumiwa anapokuwa hana imani na hakimu huomba hakimu au jaji husika ajitoe kusikiliza kesi yake.

Nne, hata katika mapungufu tuliyotaja hapo juu ya mfumo wa mahakama nchini mintarafu ya waislamu, bado mahakimu na majaji wanahukumu kesi kwa sheria za kiislamu hawana ujuzi wa kutosha katika sheria za kiislamu.

Kwa hivyo basi, majaji na mahakimu wanaoamua kesi zihusuzo sheria ya kiislamu hapa nchini hawastahiki kuhukumu kwa sheria hizo. Atahukumu vipi kwa sheria mtu asiyejua sheria hiyo? Hii imekuwa sababu kubwa ya kupindwa makusudi sheria za kiislamu katika mahakama hizi na kusambaratishwa jamii ya kiislamu. Dr. Muhammad Ali Jinah, muasisi wa Taifa la Pakistani na mwanasheria bobezi, alipata kusema:

‘The privy councils have, on several occasions, absolutely slaughtered Mohamedan law’ (Legislative Assembly Debates, Feb 1925, p.1175).

2.5.6 Njama za Kuwaritadisha (kuwabatiza) Waislamu Duniani

Katika hili kuna ushahidi wa kutosha katika kuthibitisha kuwepo kwa njama za kuwaritadisha (kuwabatiza) waislamu kupitia mlango wa sheria.

“Silent but substantial reforms through judicial activism is an unexploited field in India because they (the judges) are not militantly committed to the secular mission of the constitution… Uninhibited judicial adventure in open areas of Muslim law can be fruitful”. (VII Constitutional Assembly Debates pp 781-82, (1949).

Kwa hiyo mahakama zinakuwa zinatumika kuingilia sheria za kiislamu za ndoa, talaka, mirathi n.k. kama ilivyotokea India. Mfano;-

Mwaka 1978 Mahakama Kuu ya Allahabad ilihukumu kwamba

‘Misikiti inaweza kununuliwa kwa ajili ya matumizi ya umma. Kujengwa kwa misikiti si jambo la lazima kwa ajili ya sala kwa sababu kwa mujibu wa uislamu sala inaweza kusaliwa popote’. (Ibid).

Pia kwa mujibu wa hukumu nyingine iliyotolewa na Mahakama Kuu huko huko India

‘Makaburi ya waislamu yataheshimiwa kuwa ni makaburi pindipo yatakapokuwa yanaendela kutumika. Yakishaachwa kutumika kwa miaka zaidi ya 20, wananchi kuyavamia na kujenga au kufanya shughuli nyingine kwenye makaburi hayo watakuwa hawavunji sheria’ (Panchahat Deh V. Kucknow Municipality 1978 Allahabad, AIR, p. 280).

Vilevile katika hukumu nyingine ya Mahakama Kuu huko huko India ilihukumiwa ifuatavyo:

‘The second marriage of Muslim, is ipso facto amounts to mental cruelty for the second wife, and on its basis she can claim divorce’ (Itwari V. Asghari, AIR 1960 Allahabad, p.684.

Kwa kifupi, izingatiwe kwamba mahakama zote katika nchi za Jumuiya ya Madola (Common Wealth), Tanzania ikiwemo, hutoa hukumu dhidi ya sheria za kiislamu kwa sababu nchi hizi hutumia sheria hizi kwa pamoja (common law). Dr. Muhammad Ali Jinah, muasisi wa Taifa la Pakistani na mwanasheria bobezi, alipata kusema:

‘The privy council have on several occasions absolutely slaughtered Mohamedan law’ (Ibid).

Mifano ya athari mbaya za hukumu dhidi ya waislamu katika mahakama za hapa nchini, ni kama ile iliyotokea katika shauru la Ust. Khamis Dibagula aliyeshitakiwa na kutiwa hatiani kwa kusema Yesu sio Mungu, jambo ambalo ni sahihi kwa mujibu wa imani yake ya kiislamu. (Angalia, ‘The Muslim and State in Tanzania’ - Prof, Hamza Mustafa Njozi).

Kwa hiyo, urejeshwaji wa mahakama za makadhi ni maamuzi ya busara kufanywa na serikali kwani itakuwa inawarejeshea waislamu haki yao ya kidini na kikatiba waliyoporwa kwa muda wa miaka 45 sasa.

Na kwa kuwa, suala hili limechukua zaidi ya miaka 20 tangu waislamu kuanza kudai haki hii, kuendelea kulichelewesha ni kuwanyima waislamu haki yao, kwa mujibu wa kanuni ya kisheria isemayo “Justice delayed is justice denied”. Aidha, kwa kuwa ajenda ya mahakama ya makadhi imevutia wengi, jambo hili lisifanywe  kuwa ni ajenda ya kiisiasa, bali ni haki ya waislamu kwa mujibu wa katiba ya nchi ( 19 (1) na 20 (1 & 2).

Hata hivyo, katika mchakato wa kurejeshwa kwa mahakama za Kadhi, utaratibu wa kupatikana Makadhi na Kadhi Mkuu ni lazima usimamiwe na taasisi zote za kiislamu nchini ili kupata uwakilishi wa waislamu wote na siyo serikali au taasisi moja kupewa jukumu hilo.

V. TAMKO LA WAISLAMU

Ijumaa, Oktoba 31, 2008; Kidongo Chekundu, Dar es salaam

Ndugu Waislamu kufuatia vikao vya Masheikh, Maimamu na Viongozi wa taasisi na madhehebu mbalimbali za Kiislamu vilivyofanyika jijini Dar-es-salaam kujadili masuala ya Tanzania kujiunga na OIC na kurejeshwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini na kwa kuzingatia matamshi ya kichochezi ya Maaskofu, sisi Viongozi wa Kiislamu Tanzania tunalazimika kutoa tamko letu kama ifuatavyo:

1.    Tunasema kwamba Uislamu katika nchi hii umekuwepo kabla hata ya vyama vya siasa vilivyopo kuwepo. Pia Uislamu umekuwepo kabla ya Katiba ya Jamhuri na umekuwepo kabla ya hata Ukristo na mashirika yake ya TEC, CCT na PCT. Hatukubali kudanganywa wala kulaghaiwa na chama chochote cha siasa. Si CCM wala hicho wanachodai Maaskofu kuwa watakiunga mkono ili kuiondoa CCM madarakani kama itang’ang’ania kutekeleza ilani yake. Tunachotaraji ni kwamba Serikali iliyoko madarakani itatekeleza ahadi zake kwa wapiga kura na kuwa hatudhani kwamba utendaji serikalini unategemea matashi na ruhusa ya Maaskofu.

2.    Ni msimamo wetu kuwa suala la kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi halitategemea huruma, utashi wa Chama cha Siasa, Serikali au Kikundi cha Kikristo au asasi nyingine yeyote ile. Kwa kuwa uzawa na uraia wa Waislamu katika nchi hii hautegemei kura ya mtu mwingine yeyote, vivyo hivyo hata suala la kuwepo Mahakama ya Kadhi litakuwa ni haki ya kuzaliwa (Birth Right) ya Waislamu wa Tanzania na kuwa madhali Waislamu wanataka Mahakama hiyo basi ni msimamo wetu kuwa Mahakama hiyo itakuwepo. Aidha tunaamini kwamba pande zote zinazohusika zitatumia busara zake katika kufikia hatima hiyo kwa muda mfupi na pia kwa gharama nafuu.

3.    Madai ya Maaskofu kwamba Wakristo nao watadai kuanzisha mahakama zao kama serikali itaridhia kuanzishwa kwa mahakama ya Kadhi nchini hayana msingi ndani ya Ukristo wenyewe, kwani Biblia pia inamtambua Kadhi. Tazama Mathayo 5:25 ambayo inasema,

“Patana na mshtaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani, yule mshitaki asije akakupeleka kwa Kadhi , na Kadhi akakupeleka kwa askari ukatupwa gerezani.”

Kwa hali hiyo basi kama na Wakristo nao wanataka Kadhi wao kama huyo aliyetajwa katika Mathayo 5:25-27.Waislamu tunawaunga mkono. Sisi Waislamu tuwe na Kadhi wetu, na wao Wakristo wawe na kadhi wao.

4.    Kwa kuwa Serikali imekwishafanya uchunguzi na kujiridhisha kwamba OIC haina madhara kwa taifa bali ina manufaa mengi ya kiuchumi kama vile misaada na mikopo isiyokuwa na riba. Kwa hivyo, tunaitaka Serikali ijiunge mara moja na OIC ili wananchi wote wafaidike. Kutokujiunga na OIC kutamaanisha kuwa serikali hii inaendeshwa kwa utashi na udini wa Maaskofu.

5.    Waislamu tumeshtushwa na kauli za Maaskofu kuwa endapo serikali itaachia mjadala juu ya OIC na mahakama ya kadhi uendelee bungeni itakuwa mwanzo wa kuruhusu kuvunjika kwa amani ya nchi yetu. Kwa kauli hii ya maaskofu waislamu tunalazimika kuamini kwamba huenda maaskofu wamekwishajiandaa kuvuruga amani ya nchi hii.

Tunatoa wito kwa serikali kulitupia jicho suala hili na kufuatilia kwa karibu nyendo za makanisa haya ili kubaini mapema iwapo yana mipango ya kuvuruga amani ya nchi ili hatua zinazofaa kuepusha baa kama hilo kutokea zichukuliwe. Tahadhari hii si ya maneno matupu kwani imebainika kuwa makanisa yameshiriki kikamilifu katika vita na mauaji ya kimbari katika nchi ya Rwanda. Tunaitahadharisha Serikali kuwa ispochukua hatua mapema itawajibika kwa maafa yatakayotokea kutokana na tishio hili la uvunjifu wa amani nchini.

6.    Pamoja na kwamba Waislamu ndio walio wengi Tanzania (Tazama Sensa ya 1967 (63%), CIA Facebook 2005 (50%) na Encyclopaedia Britannica (More than 60%)), siku zote wamekuwa wakionyesha uvumilivu pamoja na kuwa wamekuwa wakibaguliwa katika elimu, ajira na madaraka serikalini na katika mgawanyo wa rasilimali za nchi. Kwa Bahati mbaya au kwa makusudi uvumilivu wetu na subira tuliyokuwa nayo vimechukuliwa kuwa ni udhaifu na unyonge katika kudai haki zetu. Tunasema kuanzia Ijumaa ya leo hatutavumilia tena ubaguzi, dharau, na vitisho vya aina yoyote ile.

Wabillahit Taufiiq

Kwa ridhaa ya Waislamu nchini, wafuatao tumesaini waraka huu.

1.    Al-Haj Abbas K. Sykes, Mwenyekiti-Dar es Salaam Islamic Club_______
2.    Sheikh Ramadhan Sanze – Katibu Mkuu- BARAZA KUU         ________
3.    Sheikh Sherali Hussein- Katibu Mkuu - BASUTA___________________
4.    Sheikh Pazi Semili- Katibu Mkuu -TAMPRO_____________________­­­­­­
5.    Sheikh Ramadhan Murtadha, Mwenyekiti wa Shura, Shia Ithnasheri___
6.    Sheikh Nassor M. Majid, Sheikh Mkuu, ISTIQAMA (Ibadhi)__________


No comments :

Post a Comment