dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, November 21, 2014

Wazanzibari wanaona giza tororo

JUU:  MUANDISHI BWNA AHMED RAJAB DURING HIS HEY DAYS AT THE BUSH HOUSE - BBC SWAHILI SERVICE!

NCHINI Chile, Amerika ya Kusini, kuna mahali panapoitwa Isla Negra (Kisiwa Cheusi).Ingawa panaitwa hivyo pahala hapo si kisiwa wala si peusi. Ni sehemu ya mwambao katikati mwa Chile na safari ya kufika huko kwa motokaa kutoka mji mkuu, Santiago, ni ya muda wa saa mbili.

Isla Negra pamepata umaarufu kwa sababu huko akiishi Pablo Neruda, mshairi maarufu wa Chile. Neruda alifariki 1973 akiwa na umri wa miaka 69. Angalikuwa bado yu hai basi Julai iliyopita angelitimia miaka 110.
Pablo Neruda alikuwa gwiji wa washairi wa karne ya 20.Sahibu yake mwanasanaa na mshairi wa Kihispania Pablo Picasso aliwahi kumuelezea hivi Neruda:
“Yeye [Neruda] si mshairi mkubwa nchini kwao tu, Chile, lakini ni mshairi mkubwa mwenye kuandika kwa lugha ya Kihispania na ni miongoni mwa washairi wakubwa duniani.”
Nimeamua kumkumbuka Neruda kwa sababu Neruda alikuwa ni mshairi wa umma aliyeyatunga mengi ya mashairi yake kuwasemea na kuwatetea wanyonge.
Yalikuwa kama ni sauti yao.
Hali kadhalika Neruda alikuwa mshairi wa mahaba, wa mazingira na wa mambo mingine. Mashairi yake ya mahaba ni matamu sana kiasi cha kumfanya Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton asifikirie kumpa mkewe Hillary zawadi yoyote nyingine kwa siku yake ya kuzaliwa zaidi ya kitabu kimoja cha Neruda cha mashairi ya mahaba.
Lakini kwa vile alikuwa mwanaharakati amepata umaarufu mkubwa kwa mashairi yake yanayogusia siasa. Na siasa zake zilikuwa za mrengo wa kushoto kulingana na uanachama wake katika Chama cha Kikomunisti cha Chile.
Neruda alikuwa pia mwanadiplomasia aliyewahi kuiwakilisha nchi yake akiwa balozi.Chile pamoja na nchi kadhaa nyingine za Amerika ya Kusini zimekuwa na utamaduni wa kuwateua washairi wake wakuu na kuwapa nyadhifa za ubalozi.
Kwa hivyo yeye aliwahi kuteuliwa balozi mdogo au balozi kamili Burma, Sri Lanka, Indonesia, Singapore, Argentina, Hispania, Ufaransa na Mexico.
Mnamo 1969 alikubali kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Kikomunisti cha Chile lakini baada ya kufanya kampeni ya nguvu kwa muda wa miezi minne akaamua kumuunga mkono Salvador Allende msoshalisti wa chama cha Unidad Popular ambaye ndiye aliyeshinda uchaguzi huo na baadaye akapinduliwa na wanajeshi walioongozwa na Jenerali Augusto Pinochet.
Allende, rafiki yake Neruda, alionyesha ushujaa alipojiua alipokabiliwa na wanajeshi badala ya kumkubalia Pinochet kwamba ampe ndege aondoke nchini aende kuishi uhamishoni.
Moyo wa Neruda na akili yake ilirowa mashairi. Unaweza kusema kwamba akinukia mashairi. Mwaka 1964 alimshangaza ripota mmoja alipomwambia kwamba kwake yeye“kuandika mashairi ni kama kuona au kusikia.”Na lazima ilikuwa hivyo kwani akiandika mashairi umri wake wote tangu akiwa mdogo sana.
Kitabu chake cha kwanza cha mashairi kilichapishwa akiwa na umri wa miaka 18. Lakini kabla ya hapo mashairi yake yakichapishwa kwenye magazeti ambamo makala yake ya mwanzo yalichapishwa alipokuwa na umri wa miaka 13.
Pamoja na mashairi Neruda aliandika vitabu kuhusu mambo mingine mbalimbali hata kuhusu mapishi. Lakini atakumbukwa zaidi kwa kuwa mshairi wa umma. Na ni mashairi yake yaliyosababisha akatunukiwa Tuzo ya Nobel ya Fasihi mwaka 1971. Akiandika kwa wino wa kijani, rangi ambayo Neruda akisema ni rangi ya matumaini.
Alipigana dhidi ya ufashisti nchini Uhispania, alipigania uhuru, usawa na haki kwa wote. Alikuwa mtu wa siasa aliyeyatumia mashairi yake kuziendeleza fikra zake za kisiasa.
Si dhamiri yangu kumwagia sifa zote Neruda bila ya kutaja mapungufu yake kwani hakuwa mwanadamu safi safina. Alikuwa na madosari yake. Kubwa ni kwamba akiwaonea wanawake. Alikuwa haziheshimu haki zao na katika mahusiano yake ya kibinafsi alikuwa akiziminya haki za wanawake aliokuwa nao. Alifika hadi hatua ya kumbaka dada wa kazi wa nyumbani kwake.
Dosari jengine la Neruda ni uamuzi wake wa kuufumbia macho ukiukwaji wa haki za binadamu katika Muungano wa Sovieti hususani pale taifa hilo lilipokuwa likiongozwa na dikteta Josef Stalin.
Ikionekana kama utawala wa kimabavu wa Sovieti ulikuwa haumshughulishi. Lakini yaliyokuwa yakijiri nchini mwake yakimhangaisha bila ya kiasi. Katika shairi moja alieleza jinsi alivyokuwa hapati usingizi, jinsi alivyokuwa akikesha akijiuliza usiku wa manane nini kitatokea Chile? Nini utakuwa mustakbali wa nchi yake maskini, iliyogubikwa na giza tororo?
Maswali kama hayo ni maswali ambayo kila Mtanzania mwenye hisia na uchungu wa taifa lake atakuwa pia anajiuliza. Ninajuwa kwa hakika kwamba Wazanzibari wanajiuliza maswali hayo kwa vile wanaghumiwa wakiwaona wakuu wao wanayashughulikia matumbo yao wakati wananchi wengi wametebwereka kwa njaa na masaibu mengine ya maisha.
Wakiangalia mbele na wakijiuliza nini utakuwa mustakbali wa nchi yao huwa wanaona giza tupu. Ni wazi kwamba Zanzibar, na Tanzania kwa jumla,ipo katika njia panda. Upande mmoja unaelekea kwenye ndoto.Upande mwingine unaelekea kwenye maafa yatayosababishwa na udikteta uliopo.
Huu udikteta uliopo ni udikteta wa kichama, wa chama kimoja kujiona kwamba pekee ndicho chenye haki na uwezo wa kutenda kitakacho.
Kuna jambo la ajabu lililotokea Tanzania baada ya kufa kwa mfumo wa utawala uliohalalisha kuwapo kwa chama kimoja tu cha siasa na kufufuliwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Nalo ni kubadilika kwa ile ndoto iliyoahidi kuwakomboa masikini na walala hoi. Hiyo ndoto sasa imegeuka na kuwa jinamizi linalolitia hofu taifa zima.
Walioigeuza hivyo ndoto hiyo ni walewale walioubadili mfumo wa chama kimoja na kuruhusu ule wa vyama vingi.
Viongozi wa chama hicho badala ya kuyaridhia matakwa ya wananchi wanazidi kuwa wachoyo, wanazidi kuwa madhalimu na wanapinga kila kinachoweza kuhatarisha madaraka yao na ulwa wao.
Hawana raghba asilani ya kuwa sehemu ya mkondo wa kihistoria utaolipatia taifa ukombozi wake wa pili baada ya uhuru — ukombozi utaowatoa kutoka kwenye minyonyoro ya siasa za ukale, ugandamizi na utawala usio wa kidemokrasia.
La kushangaza na kusikitisha ni kwamba hawa ni viongozi wa chama kilichokuwa kikisifika kwa kufuata itikadi ya ukombozi. Ni chama kilichokuwa kikijigamba kwamba kilisimama kidete kuwatetea wananchi dhidi ya ubeberu, unyonyaji na ugandamizaji wa haki zao.
Kwa kiburi chao na ukaidi wao wa kuyapuuza na kutoyajali matakwa ya wananchi viongozi hao huenda wanajiingiza wenyewe mtegoni na kulihatarisha taifa. Ikiwa wao hawayaoni hayo nadhani ni wajibu wetu kuwagutusha.
Mageuzi ya kihistoria tuliokuwa tukiyataraji hatujayashuhudia bado.Lakini siku zote umma huwa haukati tamaa. Unajuwa tu kwamba kuna siku utayashuhudia mageuzi hayo na kwamba ndoto hiyo imo mikononi mwao.
Hatari iliyopo ni kwamba ili waitimize ndoto hiyo na wahakikishe kwamba inakuwa kweli na si ndoto tena wananchi wanaweza wakaamua kumiminika mitaani.
Hiyo ndiyo hali ya mapambano.Aghalabu huzuni za wananchi huzaa mapambano. Hilo halitokuwa jambo la pekee kwa Tanzania. Neruda aliyatambua hayo alipokuwa akiitafakari hali ya Chile.
Alitambua kwamba kila taifa huwa na huzuni zake, kila mapambano huwa na maumivu yake huwa na uchungu wake. Uchungu kama ule wa mzazi.
Neruda alitupatia msamiati na sarufi inayotuwezesha kuiangalia dunia ya karne ya 21 kwa macho mengine, kwa macho mepya.
Aliwahi kusema kuwa kwa vile mashairi yalikuwepo kabla ya watu kujuwa kuandika na kupiga chapa basi mashairi ni kama mkate, na kwamba “lazima ugawanywe ili kila mtu apate kipande chake, wanaojuwa kusoma na kuandika na wakulima wadogo pamoja na wanadamu wote.”
Wakati mmoja Septemba 1972 aliwahutubia vijana akiwasimulia kuhusu maisha yake:
“Vijana lazima wajifunze kuwa vijana, na hiyo si kazi rahisi. Nilikuwa mtoto mwenye majonzi. Huzuni ya watu masikini wa kusini (mwa nchi alikokuwa akiishi), kilio cha mvua, upweke uliokataa kubadilika, yote hayo yaliyaelemea maisha yangu. Baadaye nikatambua kwamba kila maisha yanapotupa matatizo magumu, ndipo tunapozidi kupata shida za namna ya kugundua njia ya kupita.”
Hata hivyo, Neruda aliendelea kuwaeleza vijana hao, kila udhalimu dhidi ya jamii unapokuwa mkubwa ndipo tunapozidi kulazimika kufanya wajibu wetu kwa vile watawala wanakuwa wanashindwa kuwajibika. Hapo ndipo tunapoigundua njia ya kutuletea matumaini na furaha. Tunapambana ili tuweze kuisambaza furaha hiyo duniani kote.
Alipokuwa kitandani mahututi baada ya wanajeshi kumpindua Allende wanajeshi walimiminika nyumbani kwa Neruda wakipeuka kutafuta silaha. Walianza kuchimba bustanini na walipofika chumbani alikolala, Neruda alimgeukia kamanda wa kijeshi aliyewaongoza wenzake na akamwambia:
“Pekueni lakini silaha mtazozikuta hapa ni maneno tu, ni mashairi.” Yule kamanda akainamisha kichwa chake, akavua helmeti yake na akarudi nyuma huku akimwambia: “Nisamehe, Señor Neruda.”
Usiku wa pili yake Septemba 23, 1973, Neruda alifungua macho akatoa buriani kwakusema, “Me voy,” (Nakwenda) na akafa.
“Makamaradi, nizikeni Isla Negra,
mkabala wa bahari niijuayo, kila eneo lililokunjika
la mawe na mawimbi ambayo macho yangu yaliyopotea
hayatoyaona tena
Nataka kulala hapo miongoni mwa vigubiko
vya bahari na ardhi.”

No comments :

Post a Comment