dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, July 28, 2015

Lowassa: Jiwe walilolikataa CCM, kuwa jiwe kuu la upinzani?

Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Mwaka huu historia ya nchi inatarajia kurejea katika kipindi cha takriban miaka 20 iliyopita baada ya waliokuwa mawaziri waandamizi katika serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Kighoma Malima na Augustine Mrema, kujiondoa katika chama hicho na kujiunga upinzani.
Malima (marehemu) ambaye ni baba wa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, alijiondoa CCM mwaka 1995 kama ilivyokuwa kwa Mrema.
Marehemu Malima alikuwa na sifa nyingi zilizomfanya akubalike kwa watu, miongoni mwa hizo zikiwa ni jinsi alivyokuwa mkarimu, kiongozi aliyekuwa na hulka ya kuwa karibu na wananchi wa kawaida aliyekuwa na nguvu ya kupangua, kujibu na kujenga hoja.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Julai 16, 1995 wakati Tanzania ikiingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, ndipo Profesa Malima alijiengua CCM na kujiunga katika chama cha National Reconciliation Alliance (NRA) na kushiriki mkutano mkubwa wa hadhara mjini Tabora.
Kabla ya kujiondoa kwa Profesa Malima, Februari 1995, Rais aliyekuwa madarakani, Ali Hassan Mwinyi, alitangaza kumvua uwaziri aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Vijana na Ajira, Augustine Mrema, kwa kile kilichoelezwa kama utovu wa nidhamu kwa serikali.
Siku chache baadaye, Mrema alijiunga na chama cha NCCR-Mageuzi na sababu ya kujiondoa kwake kutoka CCM zikitajwa kuwa ni kukataa kwake kuwa sehemu ya fungamano la uhalifu ambao hivi sasa ni maarufu kama ufisadi.
 Mrema ambaye hivi sasa ni Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), alipinga ndani ya Baraza la Mawaziri la Rais (mstaafu) Mwinyi kuhusu wizi wa mabilioni ya shilingi yaliyotolewa kwa ajili ya kufufua zao la mkonge.
 Kashfa hiyo ikamhusisha mfanyabiashara maarufu wa wakati huo,Vidyadhar Girdharlal Chavda aliyetajwa kuwa mnufaika wa kashfa hiyo hivyo kuwa sehemu ya mabadiliko ya siasa ndani na nje ya Tanzania.
Mrema alifanikiwa kujieleza kwa umma kuhusu sababu zilizomtoa CCM, akaeleweka, ingawa kwa watawala walijitahidi kuibua propaganda ya kwamba hatua ya Mrema kujiondoa katika chama hicho ilitokana na uroho wa madaraka.
EDWARD NGOYAI LOWASSA
 Sasa ni dhahiri kwamba aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika awamu ya kwanza ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Edward Lowassa, anaondoka CCM kujiunga na upinzani, hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akiwa Chadema, Lowassa atafungamana na vyama vingine vinavyounda vuguvugu la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo ni Chama cha Wananchi (CUF), National Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi) na National League for Democracy (NLD) ambavyo tayari vimeshatoa tamko la kumkaribisha na kuahidi kumpatia nafasi (bila shaka ya kuwania Urais).
KWA NINI LOWASSA ANAHAMA CCM?
 Inawezekana orodha ya sababu zinazomfanya Lowassa kuihama CCM ni ndefu kwa kadri anavyoweza kuzielezea yeye mwenyewe, lakini zipo zilizo katika uhalisia na mazingira yanayoonekana katika siasa za kuelekea Uchaguzi Mkuu.
 Kwanza ni ukweli usiopingika kwamba Lowassa alitumia muda mrefu kujiandaa kwa ajili ya kushika nafasi kubwa ya uongozi wa nchi hii.
Itakumbukwa kwamba mwaka 1995, Lowassa alikuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliotia nia ya kutaka kuteuliwa kuwania urais. Akiwa na Rais Jakaya Kikwete (wakati huo akiwa Waziri wa Fedha), Lowassa na mshirika wake huyo wa kisiasa wakajulikana zaidi kwa jina la boys two men (Boyz II Men).
Kwa bahati mbaya, wote wawili yaani Lowassa na Kikwete hawakuteuliwa kuwania urais, badala yake nafasi hiyo ikachukuliwa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa. Hali hiyo haikuwa mwisho wa harakati na ushiriki wa siasa kwa wawili hao.
Ndio maana katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2005 ikiwa ni kipindi cha mwisho wa utawala wa Rais (mstaafu) Mkapa, Lowassa na Kikwete waliunganisha nguvu zao kisiasa, lakini tofauti na 1995, Lowassa hakujitokeza kutaka kuwania urais badala yake alimuachia Kikwete aliyeshinda na kuwa Rais wa awamu ya nne.
 Kwa maana nyingine ni sawa na kuamini kwamba Lowassa ‘hakuketi chini’ na kuachana na nia ya kuliongoza taifa hili tangu 1995. Alijiandaa na kutenda kazi kwa mfumo uliowafanya wananchi kujenga imani kwake.
Hata alipokuwa Waziri Mkuu, Lowassa alifikia hatua ya kufanya maamuzi ambayo baadaye yalisemekana kuwachukiza baadhi ya walio kwenye utawala akiwamo bosi wake, Rais Kikwete.
Hakuwa na kauli za kusubiri mchakato ama mlolongo wa uchunguzi unaoligharimu taifa fedha nyingi, bali aliwachukuliwa hatua watumishi wa umma waliobainika dhahiri kushiriki uzembe wa aina yoyote wenye kuliathiri taifa ama wananchi.
HANA MATARAJIO YOYOTE KWA CCM
Sababu nyingine inayomfanya Lowassa kuondoka CCM ni kwamba hivi sasa hana matarajio yoyote kwa CCM. Baada ya kuwa Mbunge wa Monduli tangu mwaka 1995, Lowassa amefanikiwa kushika nafasi tofauti za utumishi wa umma ukiwamo Uwaziri Mkuu ambao hata hivyo alidumu kwa kitambo tu, Desemba 2005 hadi Februari 2008 alipojiuzulu kwa kashfa ya Richmond.
 Baada ya chama hicho kumuengua katika kuwania urais mapema mwezi huu mjini Dodoma, hakuna tarajio lolote la Lowassa katika kuitumikia nchi akiwa ndani ya CCM. Labda kuendelea kuwa kimya, `akiuguza’ yaliyo moyoni mwake ikiwamo ndoto ya safari ya matumaini. Nje ya hapo hakuna!
 Kutokana na nia yake ya kulitumikia taifa katika nafasi ya Urais ‘kuzimwa’ na CCM baada ya jina lake ‘kukatwa’ katika hatua za awali kwenye Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, Lowassa alipaswa kufanya uamuzi wa aina mbili.
Mosi, kuendelea kubaki na dhamira yake huku akiwa mtiifu kwa CCM, ikibidi kuunga mkono hoja hata kama anaamini kwamba zinaiathiri jamii na taifa kwa ujumla.
Kama ingekuwa hivyo, Lowassa angejielekeza zaidi katika kulinda maslahi anayoyapata kupitia kuwapo kwake CCM na kwamba umma na mahitaji yake visingekuwa vitu vyenye maana na umuhimu kwa maisha yake.
Pili, kujiaminisha kwamba umma na maslahi ya nchi vinapaswa kutetewa, kulindwa na kuendelewa pasipo kujali mhusika yupo kwenye chama gani cha siasa.
 Sababu hiyo ndio msingi wa kufikia uamuzi wa kujiondoa CCM na kujiunga Chadema, ili kupata fursa pana ya kujieleza kwa umma, ikibidi kuonya, kukemea na kukaripia pale watawala wanapotenda kinyume cha matarajio ya walio wengi.
 Lowassa anaweza kutimiza nia hiyo kwa namna tofauti pasipo kujali kama atawania Urais ama hatapata fursa hiyo kupitia upinzani hususan Ukawa.
Ushawishi wa Lowassa kwa umma unaendeleo kutoa nafasi kubwa ya kukubalika kwake kama ilivyokuwa wakati akiwa Waziri Mkuu na hata baada ya ‘kuachia ngazi’ kutokana na kashfa ya Richmond.
Mathalan, hata alipojiuzulu kutoka nafasi ya Waziri Mkuu, Lowassa alizidi kuwavutia watu wengi waliomuunga mkono hasa katika harambee za kuchangia miradi ya maendeleo.
Licha ya kutokuwa Waziri Mkuu, bali Mbunge wa Monduli, Lowassa alifanikisha kukamilika kwa miradi mbalimbali iliyoasisiwa na taasisi za kijamii yakiwamo madhehebu ya dini na hatimaye akazidi kuaminika kwa umma kwamba anafaa kuwa kiongozi wa umma.
 Kufanikiwa huko kwa Lowassa kulirejesha historia yake alipokuwa Waziri Mkuu na katika wizara nyingine ambapo alisimamia miradi mingi ya maendeleo na ustawi wa watu, ikafanikiwa.
Miradi kama ujenzi wa shule za sekondari za kata na mradi wa maji kutoka ziwa Victoria kwenda hadi mkoani Shinyanga ni miongoni mwa sehemu ya udhihirisho wa kazi alizozifanya Lowassa.
UMMA WA WADHAMINI Vipo vielelezo kadhaa vinavyoashiria kuwa nyota ya Lowassa bado inang’ara na hivyo kuendelea kukubalika kwa wananchi walio wengi. Hatua hiyo itanufaisha upinzani kwa kufanikiwa kumshawishi mwanasiasa huyo kujiunga huko.
Mathalani, wakati wa mchakato wa kutafuta wadhamini kwa ajili ya kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais, Lowassa alipata wafuasi wengi kiasi cha kuwapo hisia kwamba walinunuliwa ili washiriki mapokezi yake.
Kila mkoa alipokwenda, watu kwa maelfu walifuatilia taarifa zake na kwenda kumpokea, kisha kumsindikiza hadi alipopata wadhamini na kuondoka katika mkoa husika. Hali ikawa hivyo kutoka mkoa mmoja hadi mwingine.
Hata orodha ya wadhamini wake ilipofika zaidi ya 800,000 kutoka 450 waliotakiwa na CCM, ikazidi kudhihirisha namna ambavyo Lowassa alivyojiandaa na alivyokubalika miongoni mwa wengi kuwa kiongozi mkuu wan chi.
Lakini hatimaye, kama ilivyonenwa kwenye vitabu vitakatifu, kwamba jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni, ndivyo inavyoonekana kwa Lowassa.
Uongozi wa CCM ulimkataa Lowassa kwa kadri ambavyo waashi walivyolikataa jiwe muhimu, wapinzani wamemchukua Lowassa kama ambavyo wasiokuwa waashi walivyolichukua jiwe lililokataliwa na kuliweka kuwa jiwe kuu la pembeni.
Je, Lowassa atafanikiwa kuiimarisha `nyumba ya upinzani’ katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu ili kuweka historia mpya kwa CCM?  
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment