dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, October 13, 2015

Lowassa aiteka rasmi Mwanza.

  Maduka yafungwa, wananchi wakesha wakimsubiri, baadhi wazimia, umati wafunga barabara ya uwanja wa ndege kwa saa kadhaa, mabomu ya machozi yapigwa.

Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa, akiwapungia mkono maelfu ya wananchi baada ya kumaliza mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu, uliofanyika kwenye Viwanja vya Furahisha mkoani Mwanza jana. Picha: Halima Kambi
Mgombea wa Urais aliyesimammishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chadema, Edward Lowassa, ameliteka jiji la Mwanza, huku uwanja wa Furahisha uliopo Ilemela ukifurika umati.
 
Mwanasiasa mkongwe nchini ambaye amejiengua CCM hivi karibuni na kujiunga na harakati za Lowassa kuwania urais, Kingunge Ngombale Mwiru ameufananisha umati huo na bahari.
 
"Hii ni bahari haijawahi kutokea... na sijawahi kuona.”
 
MJI WA SIMAMA
Kabla ya Lowassa kuwasili katika uwanja wa Furahisha alikofanya mkutano wake wa kampeni mjini hapa jana, baadhi ya wananchi walilala na kukesha katika uwanja huo ili kuwahi nafasi.
 
Aidha, maduka na sehemu nyingine za biashara zilifungwa kutokana na umati uliojitokeza kuhudhuria mkutano huo.
Awali, mamia ya vijana walijitokeza katika Uwanja wa Ndege Mwanza kwa ajili ya kumlaki mgombea urais huyo wa Ukawa, huku wengine wakipiga deki barabara alizopita kuelekea uwanja wa Furahisha.Akizungumza na wananchi hao katika mkutano wa kampeni uwanjani hapo,  Lowassa alisema ataibadilisha Tanzania kwa spidi 120.
"Na wale ambao hawawezi naomba watupishe ili sisi tuendelee na kazi," alisema.
Aidha, alisema Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo zinaweza kugharamia elimu bure na kuwalipa vizuri walimu.
 
Lowassa pia alisema atahakikisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linachukua mara nne ya sasa ya vijana ili kuongeza ufanisi katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba akiingia madarakani atahakikisha wenyeviti wa serikali, vijiji na mitaa wanalipwa posho. 
 
DUNI
Naye Mgombea Mwenza wa Urais wa Ukawa, Juma Haji Duni, alisema uongozi ni hekima na si mabavu.
 
"Kiongozi ni mwenye hekima, huruma na mwenye kujua kuwa ni kiongozi kwa sababu amechaguliwa na wananchi...sisi tunakwenda Ikulu kufanya wema na si mabaya," alisema.
 
Aidha, aliwataka wananchi hao kujiamini na kutoogopa kwani CCM lazima itaondoka madarakani.
 
"Hawa jamaa (CCM) wamechanganyikiwa na hata hawajui nini wanachokifanya," alisema.
 
Duni alidai kuna mpango unaofanywa na CCM kuiba kura ili mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli, ashinde urais uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 
Alidai ili kutimiza mikakati hiyo, serikali ya CCM imeongeza vituo hewa 24,000 vya kupigia kura na wapiga kura hewa milioni tisa.
 
"Tumewauliza Nec (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) kuhusiana na vituo hivyo hewa lakini wamekosa jibu, 'wameufyata'...ila sisi tunawaambia kuwa patachimbika," alisema.
 
KIWIA
Mgombea ubunge Jimbo la Ilemela (Chadema), Highness Kiwia, alisema watu wa Mwanza wanakilio cha muda mrefu tangu Rais Jakaya Kikwete alipowaahidi kuwajengea eneo la biashara (Machinga Complex) lakini hajatekeleza ahadi hiyo.
 
Aidha, alisema Hospitali ya Bugando imetelekezwa, haina dawa za kutosha wala vifaa tiba.
"Mheshimwa Rais (Lowassa), tunaomba utakapoingia madarakani uweze kutatua matatizo haya ya wananchi," alisema.
 
WENJE
Naye, mgombea ubunge wa Nyamagana, Ezekia  Wenje, aliwaomba viongozi wa dini kuwaombea Nec na vyombo vya usalama ili waweze kupata ujasiri wa kutenda haki katika uchaguzi mkuu.
 
MBATIA
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, alidai mgombea urais wa CCM, Dk. Magufuli akiwa Wizara ya Ujenzi alianzisha miradi 301 yenye thamani ya Sh. trilioni 5.3 lakini ameshindwa kuwalipa wakandarasi na kuisababishia Tanzania kudaiwa Sh. bilioni 124.8.
 
Aidha, aliyashukuru madhehebu ya dini nchini kwa kuwaruhusu waumini wao kwenda kupiga kura siku ya Jumapili.
"Nawashukuru sana tena sana kwa kujua umuhimu wa kupiga kura na kuwaruhusu waumini wenu kupiga kura siku hiyo... hii ina maanisha kuwa siku ya ukombozi imefika," alisema.
 
KINGUNGE
Ngombale-Mwiru  alianza kwa kuwasalimia watu: ‘Mabadilikoooo’...na kuitikiwa  ‘Lowassa’.
 
Wakati akizungumza Kingunge alishangiliwa na wananchi waliojitokeza uwanjani hapo kwa kumuita: 
 
"Babu...babu...babu, Kingunge alisema yeye anaongozwa na misingi na maadili ingawa uongozi wa CCM umevunja misingi hiyo kwa kuwanyanyasa wagombea urais 38 waliokuwa wakiwania kuteuliwa na chama hicho.
 
"Nilipoona hivyo ilibidi niondoke CCM ili niwaache waendelee kuvunja maadili...wengine walijifanya kuwa ni wafuasi wakubwa wa Hayati Julius Nyerere, walikuwa wanatamba," alisema.
 
AWATAKA CCM KUFUNGA MDOMO
Aliwataka viongozi wa CCM kufunga midomo yao na wasiendelee kumjadili baada ya kukihama chama hicho.
 
"Naomba nitamke wazi kuwa mimi nipo upande wa mabadiliko...nilianza mabadiliko hayo kuanzia Tanu hadi CCM na sasa vyama vingi...kama kuna watu wapo CCM wanahitaji mabadiliko waje huku tuungane nao," alisema.
 
AMSHANGAA MAGUFULI
Alisema anamshangaa Magufuli kwa kuahidi vitu vingi ambavyo havitatekelezeki.
"Namshangaa ndugu yangu Magufuli, ana ahadi ambazo hazifiki mwisho...hata sijui atazitekeleza vipi?" alihoji. 
 
Alisema Lowassa anatosha kuwa Rais kwa sababu ameonyesha uvumilivu kwa miaka nane.
"Ametukanwa, amepakaziwa, amezuliwa mambo lakini yeye amekaa kimya wala hawajibu...wamesahau kuwa wanazidi kumjenga kwa wananchi," alisema.
 
SUMAYE
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, aliwaomba CCM kuachia nchi kwa amani.
 
"CCM hatuhitaji vurugu, tunaiomba iachie nchi kwa amani bila vurugu zozote," alisema.
 
Sumaye alisema ataungana na Wenje Oktoba 24 mkoani Mwanza kwa ajili ya kufunga kampeni.
 
MGEJA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema huu ni muda wa Rais Jakaya Kikwete kuanza kuwaandaa wenzake kisaikolojia ili waweze kukabidhi nchi kwa wapinzani kwani wameshindwa kuongoza.
 
WATU WAZIMIA
Watu zaidi ya 60 wanadaiwa kuzimia na wengine kujeruhiwa katika mkutano huo kutokana na msongamano mkubwa katika viwanja hivyo vilivyofurika hadi barabarani.
 
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo,Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Charles Mkumbo, alisema hadi baada ya kumalizika kwa mkutano huo hakuwa amepokea taarifa zozote zaidi ya matukio mawili ya kuumia kwa watu walioanguka kutoka kwenye mti waliokuwa wamepanda na pia kupigwa kwa mabomu ya machozi kwa nia ya kuwatawanya wafuasi kadhaa wa Ukawa.
 
Kamanda Mkumbo alisema kuna watu watano wameumia na mmoja akiwa katika hali mbaya baada ya kuanguka kutoka katika tawi la mti waliokuwa wameupanda ili kufuatilia kila kinachoendelea uwanjani hapo.
 
Alisema watu hao walikimbiziwa katika Hospitali ya Sekou Toure na wanaendelea na matibabu.
 
"Hawa vijana walikuwa wamekaa katika tawi moja la mti lililoachia ghafla na kuwaangusha, wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Sekou Toure," alisema.
 
MABOMU YA MACHOZI
Katika hatua nyingine, Kamanda Mkumbo alisema polisi walilazimika kufyatua mabomu kadha ya machozi kuwatawanya baadhi ya wafuasi wa Ukawa waliokuwa wakipita mbele ya ofisi za CCM Nyamagana huku wakiwa na kila dalili ya kufanya fujo mahala hapo. 
 
Alisema mbali na matukio hayo, hakukuwa na matukio mengine ya makubwa.
 
Lowassa amebakiza mikoa miwili ambayo ni Mbeya na Pwani kukamilisha kampeni zake kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu Oktoba, 25, mwaka huu.
 
Imeandikwa na Jacqueline Massano na Daniel Mkate, Mwanza
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment