dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, October 13, 2015

Lowassa: Mwanza jiandaeni


Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa akihutubia mkutano wa kampeni katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza jana. Picha na Emmanuel Herman
By Waandishi Wetu, Mwanza
Mwanza. Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa jana alitua jijini Mwanza na kuwataka wakazi wa jiji hilo wajiandae kupokea ushindi.
Shughuli mbalimbali katika Jiji la Mwanza zilisimama wakati wa mapokezi ya Lowassa na kutokana na umati mkubwa wa watu uliofurika katika Uwanja wa Furahisha, polisi walifanya kazi ya ziada kuwapanga watu lakini hata hivyo walizidiwa nguvu.
Lowassa aliwasili kwenye viwanja vya Furahisha saa 10:20 jioni, huku akiwa ameongozana na waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale-Mwiru na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia.
Wakati mkutano huo ukiendelea idadi kubwa ya watu walipoteza fahamu kwa kukosa hewa, kutokana na msongamano na wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu walionekana wakijitahidi kuwanusuru kwa kuwatoa kwenye mkutano na kuwasogeza pembeni.
“Tumeokoa watu zaidi ya 20 walikuwa wamezimia, zaidi ni wanawake, lakini wote walizinduka baadaye,” alisema ofisa mmoja wa msalaba mwekundu.
Lowassa anayeungwa mkono na vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na NLD aliwasili Mwanza akitokea mkoani Mara, alikofanya mkutano kadhaa na kumalizia mjini Bunda na baadaye Visiwa vya Ukerewe kabla ya kutua katika Jimbo la Ilemela saa 10:20 jioni.
Kabla ya kufika kwenye viwanja hivyo, alipita angani kwa kutumia usafiri wa chopa na kuzunguka kwenye viwanja hivyo na kuufanya umati uliojitokeza kwenye viwanja hivyo kulipuka kwa shangwe huku wakiimba, “karibu rais...karibu rais wewe ndiyo mkombozi wa wanyonge pekee tunayekutegemea.”
Aliposimama kuhutubia, Lowassa aliyetumia dakika 10 kuomba kura, alisema, “kama ingekuwa tunapimwa kwa idadi ya watu, tumeshashinda, lakini tujiandae kupokea ushindi.
“Nimechoshwa na umaskini ndicho kilichonisukuma kuutaka urais,” alisema Lowassa huku akichagiza kukuza uchumi atakapoingia madarakani.
Aliahidi kuboresha hali ya maisha ya wananchi kwa kutumia raslimali zilizopo kama gesi, madini na kuimarisha kilimo kwa kuwa kinatengeneza ajira.
Duni na Serikali ya umoja
Mgombea mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji alisema kuwa amemshauri Lowassa kuwa wakiingia madarakani waunde Serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuwa Tanzania ni ya wote na kila mmoja anataka kuona Serikali yao inaleta mabadiliko.
Akizungumza na umati wa wafuasi na wanachama wa Ukawa kwenye Uwanja wa Furahisha jana, Duni alisema: “Nimemwambia Lowassa kuwa akishaapishwa, tutamchukua yeyote tunayeona anafaa kutoka chama chochote kwa ajili ya kuijenga Tanzania.”
Alisema kuwa haamini kama CCM inaweza kuleta mabadiliko na kuwataka watu wote kuichagua Chadema.
Duni pia alitumia nafasi hiyo kuishambulia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa imeandaa vituo feki vya kupigia kura kwa ajili ya kuiba kura.
Hata hivyo, tume hiyo jana ilipunguza idadi vituo hivyo kutoka 72,000 hadi 65,105 baada ya kubaini kulikuwa na makosa kadhaa katika idadi ya wapiga kura iliyotolewa awali.
Duni alisema kuwa kuna vituo hewa vingi ambavyo ikiwa mambo yatakwenda tofauti, patachambika.
Wamshukia Magufuli
Waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye alisema kuwa mgombea wa CCM, Dk John Magufuli anatumia gesi kuwagawa Watanzania baada ya kusema kuwa gesi hiyo itawanufaisha wana Mtwara na Lindi pekee.
Huku akitumia staili ya kuuliza alisema: “Hivi ninyi wa Mwanza, hamtaki gesi ya Mtwara? Kwani kinachozalishwa Mwanza ni cha Mwanza?” akajibiwa “hapanaa” na kusema: “Sasa huyo ndiyo Magufuli.”
Kwa upande wake, mshauri wa zamani wa Rais Jakaya Kikwete, Kingunge Ngombale-Mwiru aliyejitoa CCM alisema, “Magufuli ametoa ahadi nyingi na ukihesabu hazina mwisho, Magufuli hawezi kuongoza pekee kama anavyojinadi ‘Tanzania ya Magufuli’.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia aliwataka wananchi wasimchague Magufuli wala CCM.
Mbatia alizungumzia feri ya Bagamoyo iliyonunuliwa kwa Sh8 bilioni, lakini Magafuli akashindwa kulipa miradi 301 ya barabara ya Sh5.3 trilioni pamoja na deni la makandarasi linalofikia Sh124.8 bilioni pamoja na uamuzi wa jazba anaoufanya kila mara.
Akizidi kumshukia, Mbatia alisema kuwa Dk Magufuli anazungumza maneno mengi na kwamba maneno machache ya mgombea wa Ukawa ni ya busara kwani hata vitabu vya dini vinasema hivyo.

Ukerewe waomba meli
Mapema akiwa Ukerewe, wananchi walimwomba Lowassa kutatua tatizo la usafiri kati ya kisiwa cha Ukerewe na Jiji la Mwanza endapo atachaguliwa kuwa rais wa tano wa Tanzania.
Mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo la Ukerewe, Joseph Mkundi alisema kisiwa hicho kinakabiliwa na tatizo la usafiri wa meli kwa muda mrefu na kuomba alitatue.
Akizungumza na wakazi hao, Lowassa kwa kuthibitisha nia njema aliyonayo, akifanikiwa kuchaguliwa kuwa rais Oktoba 25, ziara yake ya kwanza itakuwa ya Ukerewe ili kusikiliza matatizo ya wananchi na kuyatatua.
/Mwananchi.

No comments :

Post a Comment