dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, October 13, 2015

Wagombea toeni ahadi zinazotekelezeka.

NA EDITOR

13th October 2015.
Katuni.
Taasisi ya Mwalimu Nyerere ilikaririwa na gazeti hili jana ikisema kuwa chanzo cha Watanzania kulilia mabadiliko ni kutokana na wagombea mbalimbali nafasi za uongozi kupitia vyama mbalimbali vya siasa kutoa ahadi zisizotekelezeka.
 
Kwa mujibu wa viongozi wa taasisi hiyo, Watanzania wana njaa ya kupata mabadiliko yenye tija ili kujikwamua na hali ngumu ya maisha. Siku 12 zimesalia kabla ya wananchi kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu kumchagua rais, wabunge na madiwani.
 
Maisha ya Watanzania hayawezi kukombolewa na rais peke yake, bali yanatakiwa kuanzia chini kwenye madiwani na wabunge.
 
Madiwani na wabunge ni muhimu katika sehemu ya uongozi wa nchi kwani ndiyo wanaingia kwenye halmashauri na Bunge.
 
Bunge na mabaraza ya madiwani, ni vyombo muhimu katika kuibana serikali kuleta maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini. Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unafanyika katika kipindi ambacho nchi inakabiliwa na changamoto nyingi, mathalani za ufisadi na umasikini.Ufisadi unaanzia kwenye halmashauri, ambapo ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali zimekuwa zikionyesha jinsi fedha za serikali zinavyotafunwa bila ya maelezo.
 
Ni swali la kujiuliza, inakuwaje halmashauri zinaongoza katika kutafuna fedha za umma wakati kuna madiwani waliochaguliwa na wananchi.
 
Katika kila kipindi cha uchaguzi, watu wengi wamekuwa wakijitokeza kuomba nafasi mbalimbali za uongozi na kutoa ahadi nyingi za kukwamua matatizo ya wananchi.
 
Jambo la kusikitisha ni kuwa watu wengi wanaopewa nafasi hizi za kuchaguliwa wamekuwa hawatekelezi ahadi zao na kufanya hali za wananchi kutobadilika.
 
Ndiyo maana uchaguzi wa safari hii, unatazamiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na wananchi kuchoshwa kila mara na ahadi hewa. Ni kitu cha kushangaza kuwa kuna mikoa ina rasilimali nyingi tu, lakini bado wananchi wake wamekuwa na hali ngumu ya maisha.
 
Hata hivyo, kila inapofika kipindi cha uchaguzi, wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi hujitokeza na ahadi nyingi, lakini wanapomaliza muda wao wa uongozi huondoka bila  kufanya lolote. Ni vema sasa Watanzania kutumia vizuri kipindi hiki cha kampeni kuhakikisha wanapima na kuwachambua wagombea nafasi mbalimbali za uongozi.
 
Watanzania wanapaswa kuwa macho na watu wanaojitokeza kuwania nafasi hizi za uongozi kwa ajili ya kujinufaisha.
Mathalani, kuna imani kuna watu wanaowania ubunge kwa fikra kuwa wakifika huko watanufaika kutokana na posho mbalimbali zinazotolewa huko. Ndiyo maana kuna wengine hufikia hatua ya kumwaga mamilioni ya fedha kwa kuhonga wapiga kura wafike bungeni kunufaika na fedha zinazotolewa huko.
 
Suala la ahadi zisizotekelezeka haliishii kwa wagombea wa chama tawala, bali hata wale wa vyama vya upinzani, ambao baadhi yao wameshindwa kutekelekeza ahadi zao.
 
Jambo hili la kutoa ahadi hewa, limewafanya wananchi  kujenga matumaini makubwa katika kipindi cha uchaguzi, lakini mara nyingi wale wanaopewa dhamana za uongozi hushindwa kuekeleza ahadi zao. Ni matumaini yetu kuwa katika uchaguzi wa safari hii, Watanzania watawapima wale wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi na kuhakikisha wanachagua wagombea wanaofaa.
 
Uchaguzi huu unafanyika katika kipindi ambacho Watanzania wana njaa ya maendeleo kutokana na kuwa nyuma ikichangiwa na ahadi hewa za wagombea.
 
CHANZO: NIPASHE

1 comment :

  1. continue to provide information that is useful to all who visit this blog. a visit back in jaket kulit jakarta.... thank you

    ReplyDelete