dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, April 14, 2016

YOU MUST, MUST, MUST READ THIS SPECIAL REPORT: Serikali inavyoziangamiza Muhimbili, Ocean Road

  • WAKATI serikali ikiahidi kutoa huduma bora za afya kwa wananchi, hali katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), ni mbaya kutokana na serikali kutoa kiasi kidogo cha fedha, kulinganisha na kile kinachoidhinishwa na Bunge.
Kutokana na hali hiyo, mara kadhaa wagonjwa wamekuwa wakilaumu kupata huduma hafifu huku serikali nayo ikitoa matamko kukemea na kuwafuta kazi wakuu wa taasisi hizo.

Huku hayo yakiendelea, gazeti hili limebaini kuwa changamoto nyingi zinazozikabili taasisi hizo mbili, ni ukosefu wa fedha za miradi ya maendeleo, ikiwa pamoja na kununua vifaa tiba na ukarabati.

HALI ILIVYO

Kwa mwaka wa fedha 2015/16, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, iliomba kutengewa Sh. bilioni 118.943 na Bunge likaidhinisha Sh. bilioni 1.694, lakini mpaka sasa ikiwa imebaki miezi miwili kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha, kiasi kilichotolewa ni Sh. milioni 538.

Ingawa Rais Dk. John Magufuli aliagiza kununuliwa kwa vitanda kwa ajili ya wagonjwa wa hospitali hiyo, uchunguzi umebaini kwamba MNH na taasisi zake bado zinakabiliwa na upungufu wa vitanda na wodi katika baadhi ya idara.

Katika wodi ya wagonjwa walio katika uangalizi maalum (ICU), kuna vitanda 21 badala ya 150 vinavyotakiwa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru, alisema hali hiyo inasababishwa na serikali kupanga bajeti finyu na wakati mwingine kutopata pesa za maendeleo. Katika mwaka wa fedha 2014/15, alisema mahitaji ya hospitali hiyo yalikuwa Sh. bilioni 113.25 na Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 3.8 lakini zilitolewa Sh. bilioni 1.29 tu.

Katika mwaka wa fedha 2011/12, waliomba kutumia Sh. bilioni 35.928 na Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 4.104, lakini fedha walipokea Sh. bilioni 3.762. Mwaka 2012/13, waliomba kutumia Sh. bilioni 54.804, lakini walipokea Sh. bilioni 4.625 licha ya Bunge kuidhinisha wapewe Sh bilioni 6.604.

Pia mwaka wa fedha 2013/14, walipokea Sh. bilioni 2.184 licha ya kuomba kupewa Sh. bilioni 84.691 na Bunge kuidhinisha Sh. 5.074. Kutokana na ufinyu wa bajeti ya matumizi yua kawaida (OC), Profesa Museru alisema hospitali hiyo ina malimbikizo ya madeni ambayo hadi Februari, mwaka huu, yalifikia Sh. bilioni 12.7.

"Katika miaka ya fedha 2014/15 na 2015/16, hospitali haijapata fedha za bajeti ya maendeleo," alisema Prof. Museru. Aliongeza kuwa:

"Hospitali pia ina ukosefu wa wodi za wagonjwa wanaohitaji malazi binafsi, vyumba vya madaktari, uchakavu wa majengo, barabara na mfumo wa maji safi na taka pamoja na uchache na uchakavu wa vifaa tiba.

" Pia imebainika kuwa MNH imekuwa inatumia mabilioni ya shilingi kuwahudumia wagonjwa wa msamaha kama vile watoto chini ya umri wa miaka mitano, wazee na walemavu. Huku ikipata fungu kidogo kutoka serikalini, takwimu zinaonesha katika mwaka wa fedha 2014/15, kwa mfano, hospitali ilitumia Sh. bilioni 7.2 kuwahudumia wagonjwa 89,644 wa msamaha.

Baadhi ya maeneo yaliyoathirika kutokana na uhaba huo wa fedha ni huduma na majengo kutofanyiwa ukarabati. Moja ya majengo yaliyochakaa zaidi ni la Idara ya Wagonjwa wa Akili.

Uongoziwa hospitali hiyo unasema linahatarisha usalama wa wagonjwa na watumishi. Mkuu wa idara hiyo, Dk. Frank Masao, alisema jengo hilo halijawahi kupanuliwa wala kufanyiwa ukarabati wa kuridhisha tangu mwaka 1965 lilipojengwa. Dk. Masao alisema idara hiyo ina eneo la ekari 160 lililoko Vikuruti, Mbande jijini Dar es Salaam, lakini wameshindwa kujenga majengo mapya kwa ajili ya wodi za wagonjwa, kutokana na ukosefu wa fedha.

"Mazingira tuliyonayo hapa ni magumu. "Wodi zetu hapa zimekuwa kama gereza. Wakati mwingine inatuwia vigumu kupambana na wagonjwa wa akili, hasa wale wanaopiga madaktari na wataalam wetu,” alisema."

TAASISI YA MOYO

Licha ya kuokoa fedha nyingi kwa kufanya upasuaji wa moyo nchini, badala ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoko chini ya MNH, nayo inakabiliwa na uhaba wa fedha.

Kaimu Mkurugenzi wa JKCI, Prof. Mohamed Janabi, alisema taasisi hiyo ina vyumba viwili vya upasuaji, ambavyo vimezidiwa na haijapewa fedha za miradi ya maendeleo katika mwaka huu wa fedha (2015/16).

"Katika kipindi cha Januari hadi Machi 2016, tumeona wagonjwa 17,237 na tumeokoa kiasi kikubwa cha fedha za serikali ikiwa wagonjwa wangepelekwa nje ya nchi," alisema.

Aliongeza kuwa: "Katika kipindi hicho cha miezi mitatu, tumewafanyia upasuaji wa moyo watoto 42 na watu wazima 12. Sera ya serikali inasema watoto chini ya miaka mitano watibiwe bure, lakini taasisi haijapata fungu lolote la fedha za maendeleo mwaka huu. "Gharama ya upasuaji tulioufanya mwaka huu ni Sh. bilioni 1.036.

Kama wangepelekwa Apollo (India), gharama ingekuwa Sh. bilioni 2.95.” Kutokana na hali hiyo, Prof. Janabi alisema kuna haja kwa serikali kutenga fedha ya kutosha kwa ajili ya taasisi hiyo. Alisema kwa sasa wanahitaji chumba kimoja cha upasuaji kwa kuwa vyumba viwili vilivyopo vimezidiwa.

Piawanahitaji mashine moja kwa ajili ya upasuaji wa moyo ambayo gharama zake ni dola za Marekani milioni mbili (Sh. bilioni 4.28).

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba, ambaye kamati yake ilitembelea MNH wiki iliyopita, alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 JKCI inahitaji Sh. bilioni 26 ili kujiendesha.

Hata hivyo, serikali imetenga Sh. bilioni nne kwa ajili ya bajeti ya miradi ya maendeleo ya MNH katika mwaka ujao wa fedha na hakuna fungu lililoelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya JKCI.

Kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2016/17, uliowasilishwa katika mkutano wa wabunge jijini Dar es Salaam Jumatano iliyopita na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, serikali imetenga Sh. bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na hakuna fungu lililoelekezwa JKCI.

OCEAN ROAD

Huku ikitakiwa kutoa huduma bure kwa wagonjwa wote wa saratani nchini, kwa mujibu wa sheria, ORCI nayo imekuwa ikitengewa bajeti finyu na serikali, huku fedha za miradi ya maendeleo hazitolewi kwa wakati mwafaka na wakati mwingine hazitolewi kabisa.

Takwimu za mapato na matumizi ya taasisi hiyo zinaonyesha katika mwaka wa fedha 2013/14, mahitaji yalikuwa Sh. bilioni 8.39, Bunge likaidhinisha wapewe Sh. bilioni nane (asilimia 95.3), lakini hakuna fedha zilizotolewa.

Aidha, kwa mwaka 2015/16, mahitaji ni Sh. bilioni 15.3, Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 14.9, lakini wamepewa Sh. bilioni nne, sawa na asilimia 26.8 ya kiwango kilichoidhinishwa.

Mwaka wa fedha 2011/12, ORCI iliomba kupatiwa Sh.bilioni 12.193 za miradi ya maendeleo, lakini ilipatiwa Sh. bilioni 2.5 na mwaka uliofuata (2012/13), iliomba Sh. bilioni 11.685 na Bunge likaidhinisha Sh. bilioni 3.8, lakini zilitolewa Sh. bilioni 2.8.

"Ukosefu wa fedha umeathiri huduma za taasisi, ununuzi wa vifaa na vifaa tiba pamoja na uchunguzi na tiba ya saratani nchini.

Hali hii imeendelea kulazimu wagonjwa wengi kuhitaji huduma za nje ya nchi na kuongeza mzigo kwa Serikali," alisema Dk. Julius Mwaiselage, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI.

Takwimu za taasisi hiyo zinaonyesha kuwa mahitaji ya dawa kwa 2015/16 ni Sh. bilioni 7.2, lakini serikali ilitenga Sh. milioni 790, sawa na asilimia 11 ya mahitaji halisi na zilizopelekwa hadi Machi 30, mwaka huu, ni Sh. milioni 399.5.

"Utafiti wetu wa matibabu ya saratani kwa njia ya 'Chemotherapy' (kudunga sindano), unaonyesha wastani wa gharama za matibabu ni Sh. milioni moja hadi mbili kwa mgonjwa mmoja," alisema Dk. Mwaiselage.

Hata hivyo, alisema: “Kwa fedha zilizopatikana (Sh. milioni 399.5), ni wastani wa wagonjwa 200-400 tu ambao wamepata dawa zote mwaka huu, lakini hadi Februari, mwaka huu, tulikuwa tumepokea wagonjwa wapya 3,512. Maana yake ni kwamba wagonjwa wengi (zaidi ya 3,100) hawajapata dawa.”

ITAENDELEA KESHO ......./Nipashe

No comments :

Post a Comment