dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, January 22, 2017

Barua ya Maalim Seif Sharif Hamad kwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania!

THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama cha Wananchi)
OFFICE OF SECRETARY GENERAL
P.O.BOX 3637, Zanzibar, Tanzania
Our Ref: CUF/HQ/AKM/003/017/01 Date: 11/01/2017
Mhe.Gavana,
Benki Kuu ya Tanzania (BOT),
2 Mirambo Street,
11884 Dar es salaam,
S.L.P. 2939,
DAR ES SALAAM.
YAHUSU: WIZI WA FEDHA SHILINGI 369,378,502.64 MALI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-CHAMA CHA WANANCHI)
Tafadhali husika na mada tajwa hapo juu na rejea barua ya Bodi ya Wadhamini kwako Kumb.Na.CUF/HQ/BRT/005/016/12 ya tarehe 10/10/2016.
Barua ya Bodi ya Wadhamini ya CUF-Chama cha Wananchi iliandikwa kwako kukujulisha juu ya njama zilizokuwa zikifanywa kwa ushirikiano kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na Prof.Ibrahim Haruna Lipumba kutaka kufungua akaunti katika benki ya NMB tawi la Ilala kwa minajili ya kuitumia kuiba fedha za ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi. Bodi ilifanya hivyo baada ya kupata taarifa za uhakika, ikiwemo muhtasari wa kugushi wa kikao cha Bodi kilichoketi tarehe isiyojulikana, uliotiwa sahihi na Bwana Thomas Malima na ambao ulipata baraka za Msajili wa vyama vya siasa nchini kwa barua yake yenye Kumb. Na.322/362/14/104 ya tarehe 6/10/2016. Barua ya Bodi ilinakiliwa kwa Msajili wa Hazina, Wizara ya Fedha na Wakurugenzi Watendaji wa benki zote kwa ajili ya taarifa na tahadhari. Aidha pamoja na hatua hiyo ya Bodi ya Wadhamini, nilimwandikia Msajili wa Vyama vya Siasa nchini barua Kumb.Na.CUF/HQ/AKM/003/016/023 ya tarehe 7/10/2016 kumtahadhalisha juu ya hatua yake ya kushirikiana na Prof.Ibrahim Haruna Lipumba (ambaye si mwanachama wa CUF) kuingilia masuala ya fedha za Chama ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2014) vifungu 93(1) na 98(3) yako chini ya dhamana ya Katibu Mkuu wa Chama na Bodi ya Wadhamini.
Barua hiyo niliinakili kwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NMB kwa taarifa na tahadhali na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa lolote linaloweza kutokea kutokana na njama hizo za Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na mshirika wake Prof.Ibrahim Haruna Lipumba.
Baada ya hatua hizo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini alighadhabika na kuamua bila sababu yoyote ya msingi kusitisha ruzuku ya Chama kupitia barua yake Kumb.Na.HA.322/362/14/17 ya tarehe 10/10/2016 ambayo nanukuu haya ya mwisho …. “Kwa kuwa fedha za ruzuku ni fedha za umma ambazo zinahitaji usimamizi mzuri katika matumizi yake, na kwa kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina dhamana ya kugawa fedha za ruzuku kwa Vyama vya Siasa vinavyostahili na kusimamia uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo, hivyo baada ya tafakuri ya kina nimeona ni busara kwanza kusimamisha kwa muda mgao wa ruzuku kwa chama chenu mpaka hapo chama chenu kitakaporejea katika hali shwari kiutendaji inayowezesha viongozi husika kusimamia matumizi ya fedha hizo ipasavyo.”…mwisho wa kunukuu. Sina barua nyingine toka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini inayoelekeza vinginevyo na hata kama Msajili angeliamua kuniandikia Barua nyingine kuwa anaanza kutoa tena ruzuku ya CUF kwa vyovyote vile angeliingiza kwenye akaunti ya Chama iliyoidhinishwa na Bodi ya Wadhamini kufuatia barua Kumb. Na. CUF/HQ/AKM/003/016/024 ya tarehe 14/10/2016.
Mheshimiwa Gavana, baada ya muhtasari huo wa utangulizi, kwa masikitiko makubwa leo nakuandikia barua hii kukujulisha kuwa njama za kuiba fedha za ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi zimefanikiwa kwa kufanya muamala wa jumla ya Tshs.369,378,502.64 toka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwenda akaunti Na.2072300456 ya benki ya NMB tawi la Temeke tarehe 5/1/2017. Akaunti ambayo imetumika katika wizi wa fedha hizo ilifunguliwa tarehe 01/08/2002 na viongozi wa CUF wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupokelea fedha zinazopangwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF. Ifahamike kuwa kila wilaya ya Kichama ya CUF inayo akaunti ya wilaya ambayo inatumika kupokelea fedha zinazopangwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa. Akaunti za namna hii (za wilaya) hata siku moja hazikuwahi kupangiwa matumizi ya kupokea ruzuku kutoka Serikali Kuu. Katibu Mkuu wa CUF na Bodi ya Wadhamini ya CUF, hawakuwahi kuielekeza mamlaka yoyote ya serikali na au Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba ianze kuweka fedha za ruzuku ya CUF kwenye akaunti yoyote ya CUF ya ngazi ya wilaya.
Tumejiridhisha na wizi huo na utaratibu uliotumika ni huu ufuatao;
1. Kati ya tarehe 02/01/2016 na 05/01/2017 akaunti Na. 2072300456 ilibadilisha watia sahihi kwa kuongezwa majina ya Magdalena Hamis Sakaya, Thomas Malima na Zainab Mndolwa ili watumike kuidhinisha miamala ya fedha,
2. Alhamisi ya tarehe 5/1/2017 Msajili wa Vyama vya Siasa nchini alifanya muamala wa Tshs.369,378,502.64 kwenda akaunti Na.2072300456 na watia saini wapya walikwenda kuthibitisha muamala huo kupitia tawi la NMB Mandela.
3. Ijumaa ya tarehe 6/1/2017 watia saini hao wakiongozwa na Thomas Malima walikwenda NMB tawi la Temeke na kutoa Tshs.69,000,000/= fedha taslimu na kuhamisha Tshs.300,000,000/= kwenda akaunti ya mtu binafsi Na.41401600207 ya NMB Handeni yenye jina la Mhina Masoud Omary.
4. Jumatatu ya tarehe 9/1/2017 asubuhi, Mhina Masoud Omary aliyetumika katika utakatishaji wa fedha hiyo iliyoibiwa, alikwenda tawi la NMB Magomeni na kuchukua fedha taslimu Tshs.150,000,000/= (katika mikupuo miwili ya Tshs.100,000,000/= na Tshs.50,000,000/=),
5. Siku hiyo hiyo ya Jumatatu tarehe 9/1/2017 majira ya mchana Mhina Masoud Omary alikwenda tawi la NMB Kariakoo akachukua tena Tshs.149,500,000/= (katika mikupuo miwili ya Tshs.100,000,000/= na Tshs.49,500,000/=) na akaunti yake kubaki na bakaa ya Tshs.207,907/=.
Mhe.Gavana, nyaraka za kufanyika miamala hiyo zimeambatanishwa pamoja na barua hii kwa ushuhuda na kwa hatua zako.
Tumejiridhisha kuwa huu ni wizi, utakatishaji wa fedha na ufisadi uliohusisha viongozi wa umma ikizingatiwa mambo haya yafuatayo;
a) Imekuwaje Msajili wa Vyama vya Siasa nchini asitishe ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi kwa barua Kumb.Na.HA.322/362/14/17 ya tarehe 10/1//2016 yenye nukuu …. “Kwa kuwa fedha za ruzuku ni fedha za umma ambazo zinahitaji usimamizi mzuri katika matumizi yake, na kwa kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina dhamana ya kugawa fedha za ruzuku kwa Vyama vya Siasa vinavyostahili na kusimamia uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo, hivyo baada ya tafakuri ya kina nimeona ni busara kwanza kusimamisha kwa muda mgao wa ruzuku kwa chama chenu mpaka hapo chama chenu kitakaporejea katika hali shwari kiutendaji inayowezesha viongozi husika kusimamia matumizi ya fedha hizo ipasavyo.” halafu atengue uamuzi huo bila taarifa kwa mamlaka ya Chama kikatiba kujulishwa rasmi? Inawezekanaje Msajili wa Vyama vya Siasa nchini aamue kuipa CUF ruzuku kupitia kwenye akaunti ya ngazi ya wilaya huku akiikwepa kwa makusudi, akaunti ya Chama iliyoidhinishwa na Bodi ya Wadhamini kupitia barua Kumb. Na. CUF/HQ/AKM/003/016/024 ya tarehe 14/10/2016.
b) Kama Msajili wa Vyama vya Siasa nchini alisitisha ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi kwa kutomwamini Katibu Mkuu, Kamati ya Utendaji ya Taifa, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Bodi ya Wadhamini katika kusimamia fedha hiyo, iweje akamwamini Prof.Ibrahim Haruna Lipumba na genge lake ambao anafahamu fika sio wanachama wa CUF baada ya maamuzi halali ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kumfukuzwa uanachama tarehe 27/9/2016 na kwamba shauri Na.23/2016 la Bodi ya Wadhamini dhidi Prof.Ibrahim Haruna Lipumba lililopo Mahakama Kuu bado halijahitimishwa? Je katika mazingira hayo, ushwari aliokusudia katika barua yake ya kusitisha ruzuku uko wapi?
c) Tarehe 10/10/2016 Msajili wa Vyama vya Siasa nchini alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CUF-Chama cha Wananchi yenye Kumb.Na.AB.111/368/01/77 akimtaka atenge akaunti maalum kwa ajili ya fedha ya ruzuku toka serikalini na akajibiwa kwa barua Kumb.Na.CUF/HQ/AKM/003/016/024 ya tarehe 14/10/2016 iliyoambatanishwa na muhtasari wa kikao cha Bodi ya Wadhamini kilichomjulisha kuwa akaunti maalum kwa ajili ya ruzuku ni Na. 021101002699 ya NBC Zanzibar. Kwa nini Msajili huyo huyo akafanya muamala wa fedha ya ruzuku ya Chama kwenye akaunti nyingine (akaunti Na.2072300456 ya benki ya NMB tawi la Temeke)? Nani alitengua maamuzi ya Bodi ya Wadhamini ambayo ndiyo inasimamia mali na rasilimali za Chama kikatiba?
d) Kama ilikuwa bahati mbaya, kwa nini fedha hiyo haikuelekeza kwenye akaunti Na. 011103005079 ya NBC tawi la Corporate iliyokuwa ikitumika kabla ya mabadiliko ya tarehe 14/10/2016? Lakini bahati mbaya hiyo ya kufanya muamala kwenye akaunti Na.2072300456 ya benki ya NMB tawi la Temeke, ilikuwaje ikatanguliwa na mabadiliko ya haraka ya watia saini na kuingiza majina ya watu waliokaribu na Prof.Ibrahim Haruna Lipumba kinyume na Katiba ya Chama ya 1992(Toleo la 2014) na maamuzi ya vikao halali vya Chama? Benki ya NMB imekuwaje ikasimamia na kuruhusu miamala ya viwango hivyo vikubwa vya fedha katika muda mfupi na ikizingatiwa kuwa akaunti ya Na.41401600207 ya NMB Handeni ya Mhina Masoud Omary ni ya mtu binafsi ambayo haikuwa na fedha zozote kwa muda mrefu?
e) Kitengo cha usalama cha benki ya NMB ilikuwaje kishindwe kuzingatia taratibu za kazi yao na kuzuia miamala hii ya harakaharaka mithiri ya fedha za akaunti ya ESCROW?
f) Inawezekanaje fedha za umma ambazo zinasimamiwa ugawaji na uwajibikaji katika matumizi yake kwa mujibu wa sheria za fedha za nchi na sheria ya vyama vya siasa nchini zikachezewa kwa kiwango hiki cha watu kugawana na kutolewa katika taasisi ya fedha kwa kutumia mifuko ya sandarusi bila kuchukuliwa kwa tahadhari yeyote mbali na taasisi zote za fedha nchini kujulishwa njama za Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na Prof.Ibrahim Haruna Lipumba dhidi ya fedha na rasilimali za CUF-Chama cha Wananchi kupitia barua Kumb. Na.CUF/HQ/BRT/005/016/12 ya tarehe 10/10/2016 ?
g) Baada ya fedha hizo za CUF kuhamishiwa kwenye akunti ya mtu binafsi(Na.41401600207 ya NMB Handeni ya Mhina Masoud Omary) isiyotambulika kwa Katibu Mkuu wa CUF; ambaye ndiye muwajibikaji mkuu wa masuala ya fedha kwa mujibu wa kifungu cha 93(1) cha Katiba ya CUF ya mwaka 1992(Toleo la 2014), isiyotambulika kwa Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF ambayo inawajibika kupanga bajeti mbalimbali na isiyotambulika kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF ambalo ndilo lina mamlaka ya usimamizi wa jumla wa Chama; Je Kurugenzi ya Fedha ya CUF, Wakaguzi wa Ndani wa Fedha za Chama na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) watakaguaje na kujiridhisha juu matumizi yake?
Mhe.Gavana nimekuandikia kueleza masikitiko yangu binafsi, Bodi ya Wadhamini na ya CUF-Chama cha Wananchi kwa ujumla wake kwa kitendo cha Hazina ya Wizara ya Fedha na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu na hivyo ni mjuzi katika tasnia ya sheria kwa makusudi kuacha kabisa maadili ya kazi zao na kushiriki katika utoroshaji wa fedha za Chama, kilichosajiliwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi huku wakitambua bila ya shaka yoyote kwamba kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kanuni na taratibu za masuala ya fedha na sheria za nchi. Hii ni aibu kubwa sana katika sekta ya fedha katika nchi yetu, ikizingatiwa taswira iliyoanza kujengwa na serikali ya awamu ya tano. Kama benki ya NMB inaweza kutumika katika wizi wa fedha tena za taasisi kubwa kama CUF, usalama wa fedha za serikali na za mtu mmoja mmoja zinazopitia benki hiyo ukoje? Ni nani katika Hazina ya Wizara ya Fedha anayeruhusu fedha za umma zipelekwe kokote kule bila kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za nchi? Je Msajili wa Vyama vya Siasa ni juu ya maelekezo na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusimamia rasilimali za nchi? Ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kwa fedha inayochotwa na kugawanya kwa mtindo huu unafanyikaje? Je Mamlaka ya Mapato(TRA) ilikusanya kodi kwa mnufaika Mhina Masoud Omary?
Ni maswali mengi yasiyokuwa na majibu na yenye kutia shaka juu ya uadilifu wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis S.K.Mtungi. Tunazo taarifa za Jaji Francis S.K.Mtungi kushawishi ofisi na taasisi kadhaa za serikali kugushi nyaraka ili kumnufaisha Prof.Ibrahim Haruna Lipumba na genge lake. Mwenendo huo ni hatari sio tu kwa CUF-Chama cha Wananchi bali kwa mustakabali wa siasa za vyama vingi nchini, demokrasia na utengamano wa Taifa.
Mhe.Gavana nihitimishe kwa kukuomba kwa mamlaka uliyonayo, ufuatilie na kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha kuwa fedha hiyo iliyoibiwa inarejeshwa na wahusika wote wa wizi huo, ikiwemo watendaji wa benki ya NMB waliohusika na kadhia hii wanachukuliwa hatua stahiki ili kuzuia michezo hiyo michafu inayoipotezea nchi mapato kwa vitendo viovu na ubinafsi wa watumishi wa umma wasiokuwa na maadili ya kazi zao. Kwa mamlaka yako nikuombe kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa fedha ya ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi iliyozuiliwa ambayo ni takriban Tshs.635,000,000/= inakuwa salama, na pale itakapohitajika kutolewa kwa Chama ipelekwe kwenye akaunti rasmi ya Chama iliyopitishwa na Bodi ya Wadhamini na ambayo inakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) ambayo ni A/C Na. 021101002699 ya NBC Zanzibar.
Ni matarajio yangu na Chama Chetu kuwa utazingatia taarifa hii, na maombi yetu utayapa uzito unaostahiki.
Namaliza kwa salaam za Chama chetu,
HAKI SAWA KWA WOTE
Seif Sharif Hamad
KATIBU MKUU
Nakala:
1. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali(CAG),
Makao makuu, Dar es Salaam.
2. Mkurugenzi Mtendaji National Microfinance Bank(NMB),
Makao makuu, Dar es Salaam.
3. Mkurugenzi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU,
Makao makuu, Dar es Salaam.
4. Wanasheria na Mawakili wa CUF-Chama cha Wananchi.
5. Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Makao Makuu.
Viambatanisho:
1. Barua kwa Gavana Bank Kuu, kuhusu njama za ufunguaji akaunti Kumb.Na.CUF/HQ/BRT/005/016/12 ya tarehe 10/10/2016.
2. Barua ya ufunguaji wa akaunti kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Kumb. Na. CUF/HQ/AKM/003/016/023 ya terehe 7/10/2016.
3. Barua kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kumb. Na. CUF/AKM/003/016/051 ya tarehe 14/10/2016.
4. Barua ya kufukuzwa uanachama Prof.Ibrahim Haruna Lipumba Kumb. Na. CUF/HQ/OKM/WM/2016/Vol.1/50 ya tarehe 28/9/2016.
5. Barua ya kusitishwa ruzuku Kumb. Na. HA.322/362/14/17 ya tarehe 10/10/2016

No comments :

Post a Comment